DODOMA – Watu 1,647 wamekufa katika matukio ya ajali nchini kwa mwaka 2023 huku wengine 2,716 wakipata majeraha ya muda na ya kudumu, serikali imesema bungeni mjini Dodoma.
Idadi hiyo ni sawa na vifo vya watu wanne kwa siku na ni ongezeko la vifo 102 kutoka vifo 1,545 vilivyoripotiwa mwaka 2022.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema bungeni mjini Dodoma alipowasilisha taarifa ya Hali ya Taifa ya Uchumi kwa mwaka 2023 kuwa mwaka huo ulikuwa na matukio ya ajali 1,759.
Katika matukio hayo, matukio 1,733 yalikuwa ya barabarani, majini 22 na angani 4.
Kuongezeka kwa ajali kulitokana na ubovu wa vyombo vya usafiri, uzembe wa madereva barabarani na sababu za kimazingira.
SOMA: Wanaotafuta ajira serikalini waongezeka – Ripoti
“Matukio ya ajali 1,118 yalisababisha vifo vya watu 1,647 na majeruhi 2,716 mwaka 2023 ikilinganishwa na matukio ya ajali 1,064 yaliyosababisha vifo vya watu 1,545 na majeruhi 2,278 mwaka 2022.
“Hatua mbalimbali ziliendelea kuchukuliwa kupunguza ajali za barabarani ikiwemo: ukaguzi rasmi na usio rasmi katika vituo vya mabasi, magari makubwa na madogo; kufanya doria katika barabara kuu na operesheni endelevu,” amesema.
Waziri Mkumbo ameongeza kuwa jitihanda zingine ni pamoja na ukaguzi wa shule za udereva ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya taaluma kwa madereva wa vyombo vya moto; na kuendelea kushirikiana na wadau wa usalama barabarani ili kuimarisha usimamizi wa sheria.