DODOMA – Serikali imesema imesajili watafutakazi 10,847 ikiwa ni ongezeko la watu 5,686 waliosajiliwa na kupata mafunzo ya kushindania fursa za ajira mwaka 2022.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo ameliambia Bunge leo Mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya Hali ya Taifa ya Uchumi kwa mwaka 2023 kuwa idadi hiyo ilihusisha wanaume 6,025 na wanawake 4,822.
Prof. Mkumbo amesema katika mwaka 2023, serikali kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira ilisajili watafutakazi 17,107 na kuwapatia ushauri nasaha kuhusu uchaguzi wa kazi ikilinganishwa na watafutakazi 10,540 waliosajiliwa na kupatiwa huduma ya ushauri nasaha mwaka 2022.
Ongezeko hilo ni sawa asilimia 62.3.
Hata hivyo, Serikali imesema iliendelea kutekeleza Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi kwa vijana kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
SOMA: Uchumi wa Tanzania wakua kwa asilimia 5.4
Katika kipindi hicho, Mkumbo amesema, vijana 10,220 walipata mafunzo ya ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ili waweze kuajiriwa na kujiajiri ikilinganishwa na vijana 21,586 waliopata mafunzo mwaka 2022.
Akifafanua kuhusu mchango wa miradi ya uwekezaji kwa mwaka 2023 kwenye soko la ajira, Prof. Mkumbo amesema miradi hiyo ilichangia fursa za ajira 137,010 ikilinganishwa na fursa 40,889 zilizotengenezwa mwaka 2022.
Sekta hizo ni pamoja na Miundombinu ya kiuchumi iliyotengeneza fursa 50,319, Uzalishaji viwandani (fursa 26,563), usafirishaji mizigo (18,780), kilimo (30,718), Utalii (4,103), ujenzi majengo ya biashara (3,596), huduma (1,832), madini (495) na Rasilimali watu (443).
Sekta zingine ni nishati fursa 118 na mawasiliano iliyotengeneza fursa 43.