Polisi wanawake Geita waipa tano Magereza Chato

GEITA; MTANDAO wa Polisi Wanawake (PFT-NET) mkoa wa Geita, umeeleza kuridhishwa na kuunga mkono programu ya ustadi, uwezo na maarifa inayotolewa na Jeshi la Magereza wilayani Chato kwa wafungwa.
Programu hiyo inahusisha utekelezaji kwa vitendo mkakati wa Kisayansi wa kuwajengea umahiri katika Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wafungwa na mahabusu.
Hayo yameelezwa na Kamishina Msaidizi wa Polisi mkoani Geita, ACP Adam Maro alipowaongoza polisi wanawake mkoani Geita kutoa msaada katika gereza hilo.
ACP Maro amesema PFT-NET na Jeshi la Polisi mkoani Geita linatambua nafasi ya jeshi la magereza katika kubadilisha jamii na ndiyo maana wameamua kuwapa msaada.
“Hawa ni watoto wetu ni ndugu zetu, tumeona kama jeshi la polisi suala hili linaweza kuweka alama katika mpango mzima wa kuzuia,kubaini na kutanzua kero za uhalifu,” amesema.
Amesema zawadi waliyotoa inajumuisha mahitaji ya kila siku ili kuifanya mioyo yao kubadilika kitabia kwa kuwa watafahamu namna askari hao walivyojitolea kwa upendo.
Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Wilaya ya Chato, Antony Mashauri amesema utekelezaji kwa vitendo mkakati wa Kisayansi unalenga kuwajengea umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa wafungwa.

Amesema programu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kusaidia taifa kuondokana na watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kuelekea dira ya taifa ya 2050.
Mashauri amesema kupitia mpango huo wafungwa na mahabusu 32 wanaendelea na darasa hilo ambapo wamekuwa wakipata muda wa kujifunza nyakati za jioni.
Amesema kwa sasa jeshi la Magereza haliishii kumkamata mfungwa, kumhifadhi na kumlinda bali wamegeukia stadi za urekebu na kuwajengea stadi za maisha ikiwa ni pamoja na kilimo,uvuvi na ufugaji.

Amesema katika kufanikisha mpango huo kuna mwalimu maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kawaida anayesaidiana na mwalimu ambaye ni askari katika gereza hilo.
“Tunaamini baada ya miezi mitatu mpaka sita, tutakuwa na wafungwa ambao wamekuja gerezani hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu na anatoka akiwa anamudu kusoma na stadi za maisha,” amesema.



