Polisi yajipanga Sikukuu Eid Fitri

JESHI la Polisi limesema limejipanga kuimarisha hali ya usalama wakati wa maadhimisho ya Eid al-Fitr nchini. Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema hali ya usalama nchini ni shwari na maandalizi yamekamilika kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu.

Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na viongozi katika ngazi mbalimbali za uongozi kuanzia taifa, mikoa, wilaya hadi kata ili kuimarisha usalama katika maeneo yatakayofanyika ibada za Idd, ikiwamo misikiti.

Misime ameongeza kuwa ulinzi utaimarishwa pia katika maeneo ambayo wananchi watakwenda kusherehekea sikukuu hiyo pamoja na familia, ndugu na marafiki. Aidha, amewataka wazazi na walezi kuchukua tahadhari maalum katika kipindi cha sikukuu kwa kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wote.

“Wazazi na walezi waepuke kuwaruhusu watoto kwenda kutembea peke yao bila uangalizi wa mtu mzima mwenye akili timamu ili kuepuka madhara kama vitendo vya ukatili, ajali za barabarani, hatari za kwenye fukwe na kupotea,” alisema Misime. SOMA: Wagombea zingatieni ratiba za kampeni

Pia Jeshi la Polisi liliwakumbusha wananchi kuhakikisha wanaweka ulinzi wa kutosha katika makazi yao wanapolazimika kutoka kwenda kusherehekea sikukuu ili kuepuka matukio ya wizi au uhalifu mwingine.

Vilevile, Misime ametoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria, kanuni na alama za usalama barabarani wanapotembea kwa miguu, kuvuka barabara au kuendesha vyombo vya moto, baiskeli na mikokoteni.Amesema kufuata sheria za usalama barabarani kutasaidia kupunguza ajali na kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu hiyo kwa amani na usalama.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button