PPP yaibua hoja gharama ya mlipa kodi

DAR ES SALAAM: Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) kimeibua mjadala kuhusu gharama anayoibeba mlipa kodi kutokana na Sheria ya Utumishi wa Umma, ikidai kuwa ulinzi mkubwa kwa mtumishi asiyefaa unakuwa mzigo kwa taifa.

Akizungumza jana wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Wafanyakazi kilichohudhuriwa na viongozi wa TUGHE taifa mkoa, Mkurugenzi wa PPPC, David Kafulila aliwapongeza kwa mafanikio makubwa ya kusambaza ajenda ya PPP.

“Kwa sasa Dira ya Taifa na Mpango wa Muda Mrefu (LTPP) pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDPIV) zinaonesha wazi kuwa PPP ni nguzo muhimu ya mafanikio,” alisema.

Aliongeza kuwa wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaanza, thamani ya miradi ya PPP ilikuwa Dola bilioni 1, sawa na Sh trilioni 2.5 kulingana na Mkakati wa Ufadhili wa 2021/22 – 2025/26.

“Ndani ya miaka minne, thamani ya miradi ya ubia imeongezeka kwa Sh trilioni 8.5.”

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alitoa changamoto kwa viongozi wa wafanyakazi kuhusu namna Sheria ya Utumishi wa Umma inavyomlinda mtumishi.

“Sheria iliwekwa kumlinda mtumishi dhidi ya matumizi mabaya ya viongozi wabaya. Lakini sasa inaonekana kuwa mwiba kwa mlipa kodi, kwani ugumu wa kumwondoa mtumishi asiyefaa ni gharama kubwa kwa mlipa kodi,” alifafanua.

Alitoa mfano wa Botswana ambapo mtumishi mwenye utendaji mbovu kwa miaka miwili mfululizo anafukuzwa mara moja. Endapo atakata rufaa, anaendelea kubaki nje ya utumishi hadi rufaa yake iamuliwe.

“Huko Botswana, hatua zote za kumfukuza mtumishi huchukua miezi 3 tu. Tanzania, mtumishi anakoma kuwa kazini baada ya rufaa zote kuamuliwa – mchakato unaochukua hadi miezi 22,” alisema.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Machi 2024, kati ya wafanyakazi 1,124 waliothibitika kuwa na utendaji hafifu kwa miaka miwili mfululizo mwaka 2022/23, ni watendaji 138 tu sawa na asilimia 12% waliofukuzwa. “Mfumo wa rufaa unawapa ushindi wengi.”

Kinyume chake, Botswana kwa kipindi hicho hicho cha 2022/23, kati ya wafanyakazi 241 waliothibitika kuwa na utendaji mbovu kwa miaka miwili mfululizo, watumishi 214 sawa na asilimia 88% walifukuzwa kazi.

Akirejea Ripoti ya _Oxford Review_ ya mwaka 2014, Mkurugenzi alisema kuwa asilimia 25 ya uchumi wa mataifa 13 makubwa duniani unatokana na ufanisi wa taasisi, ambao kwa kiasi kikubwa unategemea ubora wa rasilimali watu, wakiwemo watumishi wa umma.

“Watendaji wabovu wanawagharimu pakubwa walipa kodi. Ndio maana msingi wa hoja yangu kwetu wafanyakazi ni kuwa: Sheria inayotulinda dhidi ya uonevu isije ikawaonea walipa kodi,” alisisitiza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button