WAZIRI wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ameiagiza Mamlaka ya Ununuzi wa Umma ( PPRA) kuhakikisha inayaendeleza mafanikio waliyoyapata kwa mwaka uliopita ili Mamlaka hiyo iendelee kukua kila mwaka.
Dk Nchemba ametoa agizo hilo Dar es Salaam leo mara baada ya kupokea ripoti ya mwaka ya utendaji wa mamlaka hiyo ya mwaka 2023/24, ambapo ameitaka pia mamlaka hiyo kubuni vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upungufu wa bajeti.
Aidha, Dk.Mwigulu ameiagiza PPRA kuendelea kutoa mafunzo kadiri inavyotakiwa, ili kuhakikisha watumiaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki Tanzania (NeST) wanakuwa na uelewa zaidi na kuendelea kuutumia ili kudhibiti upotevu wa fedha za miradi.
SOMA: Mfumo mpya manunuzi ya umma waanza kazi
Mfumo wa NeST ulioanza kufanya kazi Julai 2023 ukilenga zaidi kusaidia kudhibiti matumizi ya fedha za serikali hasa kwenye utekelezaji wa miradi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dk Leonada Mwagike amesema kuwa pamoja na mafanikio mengine, Mamlaka ikifanikiwa kuokoa Jumla ya Sh 14.94bn/- kupitia ukaguzi na Sh 2.7tril/- kupitia ufuatiliaji.
Aidha, amesisitiza ili kuendelea kudhibiti upotevu wa fedha za miradi, Mamlaka itaendelea kuzichukulia hatua za kisheria taasisi zote ambazo hazitumii mfumo wa NeST katika ununuzi.