Prof Kabudi asisitiza majadilino kumaliza changamoto

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof Palamagamba Kabudi, amewataka viongozi wapya wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, kutumia falsafa ya 4Rs iliyoasisiwa na Dk Rais Samia Suluhu Hassan kama dira na nyenzo katika kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuimarisha demokrasia na kulisaidia Taifa.

Prof Kabudi ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 7, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa uongozi mpya na nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, uliohudhuriwa na wawakilishi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Pia Prof Kabudi amewataka viongozi hao kutumia busara na mazungumzo kuhimiza vyama ambavyo vimejitenga na baraza kurejea na kushiriki katika majadiliano, huku akisisitiza kuwa hakuna jambo lisilowezekana kupitia mazungumzo.

Aidha, amewataka kutumia majadiliano kujenga na kuibua hoja, kutafuta ufumbuzi wa changamoto na kutoa ushauri, na kwamba nguvu ya hoja ni kubwa na hivyo wadau wanapaswa kukaa pamoja na kuzungumza.

Sambamba na hayo, pia amewataka viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kanuni, huku wakitumia hekima katika maamuzi na utekelezaji wa majukumu yao, ambapo amesema viongozi mara nyingi husahau umuhimu wa misingi hiyo wanapotekeleza majukumu yao.

Amesema viongozi hao wanapaswa kutekeleza majukumu ya Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, hususan jukumu la kuvikutanisha vyama vya siasa ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu demokrasia ya vyama vingi, pamoja na kutoa ushauri unaolenga kuviweka pamoja vyama vya siasa.

Habari Zifananazo

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button