Prof Mbarawa aeleza ukuaji sekta ya uchukuzi

DODOMA: Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi wa taifa ya mwaka 2024, sekta ya Uchukuzi ilikua kwa asilimia 4.2 na kuchangia katika Pato la Taifa kwa asilimia 7.5.

‎Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Mei 13, 2026 bungeni jijini Dodoma, Prof. Mbarawa amesema kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2024, sekta hiyo imeendelea kushika nafasi ya tano kati ya sekta kubwa 17 zinazochangia Pato la Taifa.

‎Amesema Sekta ya Uchukuzi pia imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali kupitia huduma za bandari, ambapo kati ya mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2024/25, mapato yatokanayo na kodi ya forodha za kibandari yalichangia wastani wa asilimia 40 ya mapato yote yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

‎“Mapato hayo yataendelea kuongezeka siku hadi siku kutokana na maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya uchukuzi na huduma za bandari,” amesema Profesa Mbarawa.

‎Aidha, amesema sekta hiyo imeendelea kusaidia upatikanaji wa fedha za kigeni kupitia huduma za uchukuzi, usafirishaji na huduma za bandari.

‎Kwa mujibu wa Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2025, Sekta ya Uchukuzi ilichangia mauzo ya huduma yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.79 mwaka 2025, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 2.35 mwaka 2024.

‎Profesa Mbarawa ameeleza kuwa ongezeko hilo linaonesha namna sekta ya uchukuzi inavyoendelea kuimarika na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button