Prolife kuadhimisha miaka 30 ya huduma

DAR ES SALAAM; Shirika la kutetea Uhai Tanzania (Prolife) linatarajia kuadhimisha miaka 30 ya huduma zake,  huku likijivunia kuokoa mamia ya vijana, wanawake na wanaume wanaopitia changamoto za kifamilia, ndoa na maisha.

Mwenyekiti wa Prolife Tanzania, Emil Hagamu amesema Dar es Salaam leo kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia Julai 8 hadi kilele chake Julai 14, Dar es Salaam yakikutanisha watetezi wa uhai kutoka nchini na sehemu mbalimbali duniani.

Amesema hayo katika mkutano na wanachama wa Jumuiya ya Wanahabari Watetezi wa Uhai, Ndoa, Familia na Maisha (JOLIFA)- Tanzania uliofanyika Dar es Salaam.

Hagamu ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutetea uhai la Human Life International (HLI), Kanda ya Afrika kwa nchi zinazozungumza Kiingereza, amesema wageni watakaoshiriki maadhimisho hayo ni pamoja na maaskofu, mapadri, wawakilishi kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na wadau wengine kutoka Lesotho, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Kenya, Marekani, Ireland na Malawi.

“Tunatumia nafasi ya maadhimisho haya kumshukuru Mungu kwa utume wetu uliodumu kwa miaka 30. Kuna mashirika mengi tulianza nayo lakini yamekufa kwa kuwa hayakuwa na mizizi wa utume, sisi muda wetu mwingi ni kujitolea,”amesema.

Kwa mujibu wa Hagamu, miongoni mwa matukio muhimu yatakayofanyika ni pamoja na mijadala na tafakari kuhusu Utume wa utetezi wa Uhai Tanzania, familia, ndoa, vitisho vinavyokabili Kanisa na program za Prolife.

Matukio mengine ni uzinduzi wa kitabu cha historia ya Prolife Tanzania, utoaJI wa zawadi na tuzo kwa taasisi na watu waliofanya vizuri katika utume wao, kupanga mikakati ya miaka 30 na kuzuru Bagamoyo ambayo ni lango la imani.

Amesema katika miaka 30 ya utume wao, wamefanikiwa kusaidia wanandoa kubaini changamoto zao likiwamo suala la kupanga mpishano wa watoto bila kutumia njia hatarishi za kiafya, kisaikolojia na zinazokwenda kinyume na mafundisho ya imani juu ya uumbaji na mambo mengine mbalimbali.

Hagamu amesema wameanzisha programu nyingine kuwaelimisha vijana walioko shuleni na katika vyuo kuhusu namna ya kutambua tunu zao ambazo ni upendo, heshima, adabu, utii, kazi, usafi wa moyo na imani na uzalendo.

Programu nyingine walizofanikiwa kutekeleza ni pamoja na unasihi na uponyaji kwa watu wanaoteseka na msongo wa kimaisha kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya na utoaji mimba.

Habari Zifananazo

Back to top button