Putin yuko tayari kumaliza vita Ukraine

MAREKANI : RAIS wa Urusi Vladimir Putin amempongeza Donald Trump kwa ushindi wake wa uchaguzi huku akimtaja ni mtu jasiri.

Akizungumza katika mji wa Sochi nchini Urusi, Putin amesema kuwa Trump hapo awali alidhulumiwa kutoka pande zote katika muhula wake wa kwanza katika Ikulu ya White House.

Putin amesema madai ya Trump ya kutaka kurejesha amani Ukraine yanapaswa kuzingatiwa kwa ukaribu.

Advertisement

Wakati wa kampeni yake, Donald Trump alisema mara kwa mara kwamba anaweza kumaliza vita hiyo.

Wakati wa hotuba hiyo, Putin alizungumza kwa saa kadhaa akiangazia mada tofauti. Pia alizungumzia jaribio la kumuua Donald Trump mwezi Julai, alisema lilimvutia sana.

Baada ya kupigwa risasi, Trump aliinua mkono akiwa amekunja ngumi hewani na kusema maneno “pigana, pigana, pigana”, kabla ya kuondolewa katika eneo la tukio na maafisa wa huduma ya usalama.

“Kwa mtazamo wangu, alionyesha ujasiri,” Putin alisema.

Alipoulizwa ikiwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Donald Trump, Putin alijibu: “Tuko tayari, tuko tayari.”

Siku ya Alhamisi Trump pia alinukuliwa akisema yuko tayari kuzungumza na Putin.