Rais mpya Chad aapishwa

N’Djamena, CHAD: RAIS mpya wa Chad, Mahamat Idriss Deby, ameapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo, baada ya miaka mitatu kama kiongozi wa mpito wa kijeshi.

Muda mfupi baada ya kuapishwa, alimtangaza Allamaye Halina kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, baada ya Succes Masra kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo wiki hii.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/waziri-mkuu-wa-chad-ajiuzulu-baada-ya-mshindi-wa-kura-kuthibitishwa/

Akizungumza katika sherehe ya kuapishwa katika mji mkuu wa N’Djamena Alhamis, ambayo ilifuatia uchaguzi uliokuwa na mabishano mapema mwezi huu, Deby alisema: “Kwa ndugu na dada zangu ambao hawakunichagua … ningependa kusema kwamba ninaheshimu uchaguzi wenu, ambao unasaidia katika maisha ya demokrasia yetu”.

Deby alipata asilimia 61 ya kura za Mei 6, ambazo mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa yalisema hazikuwa za kuaminika wala huru.

Alitangazwa kuwa Rais wa mpito mnamo Aprili 2021 baada ya waasi kumuua baba yake, Idriss Deby, ambaye alitawala Chad tangu mapinduzi mapema miaka ya 1990.

Deby aliidhinishwa haraka kama kiongozi wa mpito na jumuiya ya kimataifa inayoongozwa na Ufaransa, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imeondolewa na serikali za kijeshi katika makoloni ya zamani ya Mali, Burkina Faso na Niger. Ufaransa kwa sasa ina askari 1000 nchini Chad.

Kuapishwa kwake kuliashiria mwisho wa miaka mitatu ya utawala wa kijeshi katika Chad yenye utajiri wa mafuta, lakini ni moja ya nchi masikini zaidi barani Afrika. Masra, ambaye alijiuzulu wadhifa huo Jumatano, alikuwa mpinzani mkuu wa Deby katika uchaguzi huo.

Alikuwa Waziri Mkuu tangu mwanzo wa mwaka, baada ya kurudi nchini chini ya makubaliano ya upatanisho baada ya kipindi cha uhamisho kufuatia kukandamizwa kwa maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi. Kiongozi huyo wa upinzani alichukua nafasi ya pili katika uchaguzi huo akiwa na asilimia 18.54 ya kura.

 

Habari Zifananazo

Back to top button