Rais Mwinyi asaini sheria 4 ikiwemo ya Kadhi

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesaini sheria mpya nne kwa mara ya kwanza ikiwemo Sheria ya Kadhi ya mwaka 2023  ambayo imefuta  sheria namba  09 ya mahakama ya kadhi ya mwaka 2017.

Amesema sheria hizo zitaondoa changamoto ambazo zilikuwa vikwazo katika kufikia malengo ya kimaendeleo.

Sheria hizo mpya zilizosainiwa leo ni Sheria mpya ya Mahakama ya Kadhi Zanzibar, Sheria mpya ya Ukaguzi wa Umma, Sheria mpya ya Uwekezaji Zanzibar.

Advertisement

Amesema, sheria hizo ni  bora kwa mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji nchini, Sheria ya kuweka masharti ya  utoaji leseni udhibiti na usimamizi wa huduma ndogo za fedha kwa ajili ya kudumisha utulivu, usalama na ubora wa huduma hizo.

Rais Mwinyi amesema hayo wakati wa  hafla ya utiaji saini wa sheria mpya nne viwanja vya Ikulu Zanzibar leo Februari Mosi,  2024.

Aidha Rais amesema sheria zilizosainiwa zimepita katika hatua mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa utafiti wa kina na ukusanyaji wa maoni ya wadau Unguja na Pemba kabla ya kuwasiilishwa  Baraza la Wawakilishi na kujadiliwa kwa mfumo wa demokrasia shirikishi.

Amesema, ni jambo la kihistoria kusainiwa kwa sheria mpya nne hadharani kwa wakati mmoja.

Rais Mwinyi amesisitiza kuwa sheria zote nne zilizosainiwa zinagusa moja kwa moja maslahi ya wananchi na haki zao ikiwemo kuimarisha miongozo ya mifumo jumuishi ya  kusimamia shughuli zote za uwekezaji.

Pia, kupanua wigo wa kazi za ukaguzi  ili kufikia ngazi za kitaifa na kimataifa, kubaini na kuzuia matumizi mabaya ya fedha za umma, kukabiliana na vitendo vya rushwa, kuzuia matumizi  mabaya ya mifumo inayoathiri utekelezaji wa kazi za ukaguzi.

Rais Dk.Mwinyi amezitaka taasisi za sheria kufanya mapitio ya  sheria zinazokwaza kasi ya maendeleo katika maeneo ya mafuta na gesi asilia.