Rais Samia ampongeza Askofu Rugambwa
Ni kwa kuteuliwa kuwa Kardinali
RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Protase Rugambwa kwa kuteuliwa na Papa Fransisco kuwa Kardinali
Akitoa pongezi hizo Rais Samia amesema, “Naungana na Watanzania wote kukutakia kheri na kukusindikiza katika sala, unapoendelea na kazi yako ya utume katika hatua hii mpya. Mwenyezi Mungu ambaye amekuinua kwa baraka na jukumu hili kwenye wito wako, aendelee kukuongoza katika kulitumikia Kanisa na jamii yetu kwa ujumla.
Pongezi hizo za Rais Samia, zimekuja saa chache baada ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Fransisco kutangaza kumteua Askofu Rugambwa kuwa kardinali.
Askofu Rugambwa na Maaskofu wengine 17 kutoka Juba Sudani Kusini, Brazil, Hong Kong, Bagota Colombia, Lisbon Ureno na Lodz Poland watasimikwa rasmi Septemba 30, 2023
Akitangaza uteuzi huo leo Julai 9, 2023 Papa Fransisco amesema “Ningependa kutangaza kwamba Septemba 30, nitawasimika makadinali wote wapya waliopata uteuzi. Wanakotoka kunaonyesha umoja wa Kanisa, ambao unaendelea kutangaza matendo ya huruma ya Mungu kwa watu wote wa dunia.
Aidha Papa Fransisco amesema kuteuliwa kwa Makardinali wapya katika Jimbo Kuu la Roma, kunadhihirisha mshikamano usioweza kutenganishwa kati ya Kiti cha Petro na Makanisa yaliyoenea duniani kote.
Askofu Rugambwa anakuwa kardinali wa tatu kutoka Tanzania ambapo wa kwanza alikuwa Laurean Rugambwa akifuatiwa na Polycarp Pengo.
Askofu Rugambwa aliwahi kuwa askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2012 pamoja na Katibu Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji Vatican.
Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican News, Askofu Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 mkoani Kagera na kabla ya kupata daraja la upadri alisoma katika seminari ndogo za Katoke, Jimbo la Rulenge-Ngara na Itaga mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican News, Askofu Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 Bunena-Bukoba nchini Tanzania, akapata Daraja Takatifu la Upadri kutoka mikononi mwa Mtakatifu Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania Septemba 2,1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara.
Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican.
Papa Benedikto XVI, Januari 18, 2008 alimteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na Juni 26, 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu Mkuu.
Novemba 9, 2017 Papa Fransisco alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baada ya kulitumikia baraza kwa vipindi viwili na muda wake ukafika ukomo kwa mujibu wa Katiba.
Aprili 13, 2023, Papa Fransisco alimteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu Mkuu kurithi Jimbo Kuu la Tabora, Tanzania.