Walimu watakiwa kukabili mimba za utotoni

MANYARA: Walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani Babati mkoani Manyara wametakiwa kuanzisha klabu za maadili ya watoto ili kuwa na taifa bora, kupiga vita mimba za utotoni na utoro shuleni.
Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Mariam Muhaji, ametoa agizo hilo Aprili 21, 2026 wilayani Babati wakati wa mafunzo ya uanzishwaji wa klabu za maadili yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini.

”Uanzishaji wa klabu za maadili haya utasaidia sana kukuza maendeleo ya mkoa na kuongeza kiwango cha ufaulu mkoani Manyara,” amesema Muhaji na kuongeza: “Zitasaidia kupunguza utoro shuleni,mimba za utotoni na kitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto”.
Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Gerald Mwaitebele, amesema kuwa suala la maadili likitiliwa mkazo kuanzia shuleni, jamii itapata viongozi bora.



