DAR ES SALAAM; RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza mbunifu wa mavazi Mtanzania Anjali Borkhataria kwa kuiwakilisha nchi vizuri kimataifa kwenye masuala ya ubunifu, kujituma na uthubutu wake.
Rais Samia ametoa pongezi hizo leo kupitia mtandao wa Instagram kwenye ukurasa wa mbunifu huyo baada ya kuona sehemu ya mahojiano yake na moja ya kituo cha redio nchini.
“Binti yangu Anjali wasaidizi wangu wamenionesha sehemu ya mahojiano yako. Hongera kwa ubunifu hasa wa nakshi za Afrika na Kiswahili kwenye kazi zako, kujituma, uthubutu na kushirikiana na vijana wenzako kwenye kazi, nimesikia ndoto yako, wasaidizi wangu watawasiliana na wewe,” ameandika Rais Samia.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/mtanzania-aweka-rekodi-ufaransa/
Rais Samia amesema wanaendelea kuweka mazingira bora ya vijana wengi kujituma na kufanikiwa kupitia ubunifu na sekta zingine. Amesema anafurahishwa kuona idadi ya vijana wanaopiga hatua na kuboresha maisha ikizidi kuongezeka.
Hatua hiyo imekuja baada ya Anjali Borkhataria kusema kuwa anaAndaa vazi kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan litakalokuwa na nakshi za Kiswahili likielezea asili na tamaduni za Kitanzania.
Amesema pongezi hizo ni wazi kuwa serikali inaunga mkono vijana ambao wanafanya kazi kwa bidii kutimiza ndoto zao. Amesema ahadi ya Rais Samia imempa matumaini na kuamini kwamba ndoto yoyote inaweza kufikiwa kupitia juhudi na kujituma.
“Ahadi yake ya kutimiza ndoto yangu ya kumvalisha inadhihirisha kwamba kazi yangu inathaminiwa na inatambulika hata na viongozi wa juu wa nchi. Hili linanipa motisha na ari mpya ya kuendelea na juhudi zangu za ubunifu,” amesema Anjali.
Juni 25, 2024 mbunifu huyo aliiheshimisha nchi baada ya kuwa mbunifu wa kwanza kutumbuiza kwenye onesho la ‘pop-up’, lililoandaliwa na Galeries Lafayette nchini Ufaransa.