RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kuongeza saa 24 za uokoaji katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo.
Katika taarifa ya Ikulu Rais Dk. Samia ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza kwa njia ya simu kutoka Brazil na Waziri Mkuu Majaliwa kuhusiana na zoezi la uokoaji na kusema: “Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalum wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuweza kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo.
SOMA: Tume kuchunguza ubora wa maghorofa Kariakoo
Ninakupa maelekezo ya kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi ili kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai.”
Aidha, Rais Dkt. Samia pia ameongeza kusema kuwa: “Kwa vikosi vyetu vyote na wananchi wote wanaopambana kuokoa maisha ya ndugu zetu katika zoezi hilo ninaomba ufikishe salamu zangu na uwaeleze kuwa natambua na nina wathamini sana. Wameonyesha utu, uzalendo mkubwa na uchapakazi wa hali ya juu sana. Hivyo nawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania ndugu zetu kwani ninyi ni mashujaa wa taifa letu.”
Rais Dk. Samia anawaombea kwa Mungu awalinde na kuwapa nguvu muda wote wakiwa wanateleleza jukumu hilo kubwa na la kizalendo.
Kwa upande mwingine, Rais Dk. Samia amewasihi wananchi, ndugu na jamaa kuendelea kuwa na subira na kama taifa tuendelee kuwaombea ndugu zetu na wapiganaji wetu ili kufanikishe zoezi hilo kwa mafanikio makubwa.
“Mwenyezi Mungu tunakuomba utufanyie wepesi kwenye zoezi hili. Amin,” amesema Rais Dk. Samia.