Rais Samia ataka nidhamu kwa watumishi wa Umma
MANYARA: Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watumishi wa Umma kuwa na nidhamu katika utendaji kazi wao kwa Wananchi ili kuondokana na Malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara katika Taasisi mbalimbali.
Rais, Samia ameyasema hayo leo Oktoba 14 katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 zilizofanyikia katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo katika mji wa Babati mkoani Manyara.
“kumekuwa na malalamiko ya Wananchi kuhusu matumizi ya lugha chafu, kucheleweshwa kwa huduma au kudaiwa rushwa na hili ninawataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya mlibebe ipasavyo maana huko chini ndio kwenye shida kubwa” amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa ya kilimo biashara, kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza tatizo la ajira nchini
Kwa upande wake Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema kuwa jitihada za makusudi za utunzaji wa mazingira zinahitajika ili kulinda na kutunza mazingira kwa vizazi vijavyo.
Akiwakilisha salamu za Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema zaidi ya Sh bilioni 535.7 zimetolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya maji,barabara Elimu pamoja Afya.
Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2024 utazinduliwa mkoani Kilimanjaro na kilele cha mbio hizo pamoja na wiki ya vijana itafanyika mkoani Mwanza.