ZANZIBAR; RAIS Samia Suluhu Hassan amemtaka bosi mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph
Mwenda kuhakikisha anaziba mianya ya wizi na ukwepaji kodi ili mapato yakusanywe kwa wingi kuepuka unyanyasaji kwenye mikopo.
Amesema aliyekuwa Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata amefanya vizuri katika ukusanyaji kodi kufikia Sh trilioni 27, lakini amemuondoa kutokana na kuandamwa.
Akizungumza jana Ikulu ya Tunguu, Zanzibar baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia alisema amemuweka Mwenda kwa kuwa yeye ni kijana wa mjini Dar es Salaam na anajua uhuni wote unaofanyika TRA na pengine aliwahi kushiriki.
Alisema Mwenda anajua mipango yote ya kupenyeza bidhaa kutoka bandarini hivyo alimtaka kwenda
kuziba mianya hiyo kwani wanachohitaji ni mapato na kuepuka kukopa.
“Tumekuwa tukikopa na wakati mwingine tunanyanyasika lakini hatuachi kwa kuwa tuna miradi ya maendeleo inayohitaji fedha Hivyo, twende tukanyanyue za kwetu,” alisisitiza.
Alieleza serikali imefanya yote ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji lakini tatizo
lililopo ni kulipa kodi.
Alisema Kariakoo peke yake wakikusanya mapato ipasavyo yanaweza kuendesha wizara tatu lakini sasa
hazikusanywi kwenda serikalini badala yake huwekwa mifukoni.
“Yaliyofanyika ndani yote unayajua…nenda kazibe tunahitaji fedha, nimekuamini na najua utakwenda kufanya
kazi,” alieleza.
Rais Samia alieleza kuwa watu watafurahi kuwa wanamjua hivyo kama anataka kukaa ageuze uso.
“Kidata hakuwa mpenzi kabisa kwa sababu alipotakiwa kuingiza mizigo bila kulipa kodi alikataa, hata sisi
tulikuwa hatumpendi. Wewe kuwa mzuri kwetu sisi tuliokuteua na utafanya kazi ukusanye fedha,” alisema.
Akizungumzia maboresho, alifafanua kuwa bandarini kuna maboresho makubwa kwani ameweka
wawekezaji na kuna meli nyingi zinazoingia hivyo wakisimamia vizuri wanaweza kuendesha bajeti ya nchi
nzima.
“Tayari mwenzako amefanya vizuri kwani baadhi ya mifumo inasomana na mingine ilikuwa bado lakini
nimemuondosha anakuja ofisini kwangu na kazi yake kukufuata mgongoni na anafahamu vichochoro vyote vya TRA,” alieleza.
Aliongeza: “Usitake kupendwa na watu hakikisha wanalipa kodi hata kama mtu anaitwa Suluhu, watu walipe kodi hata wakikwambia mimi ndugu yao, tumechoka kunyanyasika kwa kukopa.”
Uhusiano na wafanyabiashara
Rais Samia alimtaka Mwenda kuhakikisha wanakuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara
ili waweze kulipa kodi licha ya kwamba kwa asili yao hawataki kulipa kodi.
“Nimekuamini umefanya vizuri Zanzibar katika kukusanya kodi. Nchi nzima matumizi ya mashine za
kielektroniki hazitumiki, mtafanyaje kutumika kwa mashine hizo ili kulipa kodi mchemshe bongo muone
mnafanyaje,” alisema.
Alieleza kuwa wafanyabiashara ni wepesi kulalamika na kuchafua siasa lakini wanakusanya kodi ya ongezeko
la thamani (VAT) lakini hawapeleki TRA, wanadanganya ritani hivyo wanapaswa kuwa makini wanapowachukulia hatua ili kodi zilipwe.
Rais Samia alisema Kidata ameokoa Sh bilioni 60 kwa vitu ambavyo vilipaswa
kulipiwa kodi lakini vilikuwa vinapenyezwa kwa njia ya panya.
Alisema mapato ya ndani yasiyo ya kodi yamepanda lakini bado halmashauri hazipeleki kodi inavyopaswa kwani wanatengeneza mifumo miwili ya kukusanya kodi hivyo, alimtaka kufuatilia na kuhakikisha
halmashauri zinakuwa na mfumo unaoeleweka wa kukusanya kodi.
“Umepewa dhamana kubwa nenda kafanye kazi kwa kuweka maslahi ya taifa mbele. Wakati mwingine
CAG anakuja na queries (maswali) ambazo hazikuwa na haja watu wanajisahau na wanafanya wawezavyo, tukifanya kazi vizuri haya maswali hayawezi kuwepo,” alisisitiza.
Vilevile alisema ni muhimu viongozi hao kushirikiana baina yao kwani hakuna wizara ya mtu, sekta zote zinashabihiana hivyo wawasiliane ili mambo yaende haraka kwa kuwa wote wanajenga Tanzania.
“Cheo ni dhamana ndugu zangu na si mali ya mtu, ni utumishi wa serikali kwa watu wake hivyo sisi tuliochaguliwa kutumikia watu twendeni tukafanye, tutaulizwa na Mungu tusipotimiza wajibu wetu,” alisema Rais
Samia.