Rais wa Finland ashukuru Watanzania

RAIS wa Finland, Alexander Stubb ameshukuru Watanzania kwa ukarimu wao katika mapokezi aliyopata kwenye
ziara ya kitaifa ya siku tatu aliyoianza nchini Mei 14.

Stubb amesema upendo wa Watanzania unaendelea kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo zilizokubaliana kuongeza ushirikiano kwenye sekta mbalimbali.

Alisema hayo alipotembelea makumbusho ya taifa Dar es Salaam na kuona utunzaji wa historia, urithi na malikale zinazoonesha asili, chimbuko na vifaa vilivyotumika kwenye historia ya binadamu na hifadhi za rasilimali bahari.

“Asanteni sana Watanzania kwa ukarimu mzuri tulioupata katika ziara hii ya kitaifa, nafurahi pia kutembelea Makumbusho ya Taifa. Mke wangu alikuwa hapa jana (juzi) akasema ni mahali pazuri sana, pana mpangilio, nimejua chimbuko la binadamu, sasa najua asili yangu ni wapi,” alisema Rais Stubb.

Alisema Finland na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu na kupitia makumbusho hiyo wataendeleza uhusiano na kwenye maeneo yenye fursa za ushirikiano.

“Nilikuwa nikijiuliza nitaitangaza vipi Finland baada ya kuona Mlima Kilimanjaro, baada ya safari ya wanyamapori na baada ya Zanzibar. Lakini mkipata nafasi ya kuitembelea Finland ningependekeza mtembelee vivutio vyetu yakiwemo maziwa, vivutio hivi naamini vinatuunganisha kwenye upande wa utalii,” alisema Rais Stubb.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alisema mataifa hayo yamebaini fursa zilizopo za ushirikiano katika maeneo sita yanayohusu urithi wa kitamaduni, uhifadhi wa viumbemaji na mazingira.

Alisema ziara hiyo ni ukumbusho wenye maana kuhusu fursa zilizopo mbele yetu kwa ajili ya kulinda, kuendeleza na kushirikiana katika urithi wa kitamaduni.

Aliongeza, “Tanzania inathamini utajiri wa utamaduni na urithi wa kihistoria na ziara hii imebaini fursa ya uwezekano wa kuimarisha ushirikiano na Finland katika maeneo ambayo yatasaidia si tu kulinda urithi wetu, bali pia kukuza maarifa na kubadilishana tamaduni kati ya nchi zetu,” alisema.

Dk Chana alitaja maeneo yenye fursa ya ushirikiano ni kuanzisha programu za pamoja za kuwajengea uwezo
wataalamu wa urithi kutoka nchi hizo mbili.

Eneo lingine ni kuanzisha ubia wa kuendeleza makumbusho zinazotembea za kidijiti kwa njia ya simu ili jamii ifikiwe na historia hiyo ambayo ikibaki ndani ya makumbusho haitawafikia wengi walio nje.

Alitaja eneo lingine ni kuimarisha uhifadhi wa urithi wa baharini, kwa ajili ya utafiti, elimu kuhusu historia ya binadamu na hatua zake kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Lingine ni kufanya tafiti za kisayansi kwa ajili ya uvumbuzi na kujifunza kwa pamoja kati ya taasisi za mataifa hayo za makumbusho.

Dk Chana alitaja eneo lingine ni kutumia teknolojia za kisasa kuonesha uhalisia ulioboreshwa na michoro ya 3D ili kuimarisha uzoefu wa urithi wa kitamaduni.

Alisema pia, kuna fursa ya kuimarisha na kuhifadhi urithi wa kihistoria uliyopo kwenye nyaraka ili kulinda kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button