Rasilimali Saccos zafikia tril 1.69/-

DAR ES SALAAM: VYAMA vya kuweka na kukopa (SACCOS) nchini vimeongeza rasilimali zake kutoka Sh trilioni 1.4 hadi Sh trilioni 1.69, huku akiba na amana za wanachama zikiongezeka kutoka Sh trilioni 1.01 hadi Sh trilioni 1.22, hatua inayoonesha kukua kwa sekta hiyo katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha anayeshughulikia Usimamizi wa Fedha, Asha Khamis Abdulla na Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo, leo kwenye Kongamano la 26 la Shirikisho la Afrika la Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCA), lililofanyika Dar es Salaam, ambapo walizitaka SACCOS kuelekeza huduma za kifedha katika shughuli za uzalishaji.

Wamesema huduma za mikopo kwa gharama nafuu ni muhimu kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kuwekeza katika pembejeo, teknolojia za kisasa, mitambo, usindikaji wa mazao na masoko ili kuongeza kipato na ajira.

Wamesema hadi Desemba 2025, idadi ya SACCOS zilizopewa leseni Tanzania ilifikia 981 kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, zikiwa na wanachama na wanufaika wapatao milioni 1.9 na rasilimali za Sh trilioni 1.206. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alisema idadi ya SACCOS zilizopewa leseni iliongezeka kutoka 884 hadi 1,016, huku wanachama wakifikia milioni 1.9.

Wamesema zaidi ya asilimia 92 ya fedha zinazotumiwa na SACCOS zinatokana na michango ya wanachama, hivyo ni muhimu kulinda akiba hizo kupitia utawala bora, uwazi na usimamizi madhubuti wa fedha.

Wamesema serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa SACCOS kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), kuhimiza matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika uanachama, uongozi na fursa za kiuchumi.

Wamezitaka SACCOS na wadau wa Afrika kutumia kongamano hilo kubadilishana uzoefu na kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya wanachama, chini ya kaulimbiu: “Kujenga Imani, Kuchochea Mabadiliko: Mustakabali wa Vyama vya Ushirika wa Kifedha Afrika.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button