MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameridhishwa na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali Za Mitaa katika uchaguzi uliofanyika leo.
Akizuzgumza katika kituo cha Mtendaji wa Kata ya Mjini, Mtaa wa Shede Manispaa ya Kigoma Ujiji Mkuu huyo wa mkoa amesema licha ya kuridhishwa na idadi kubwa, lakini pia upigaji kura umekuwa wa amani na utulivu.
Katika hatua nyingine wananchi katika maeneo ya wilaya mbalimbali Kigoma wamejitokeza kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa huku wakieleza kuridhishwa na taratibu zilizopo vituoni ambazo zimewezesha kupiga kura kwa amani, usalama bila usumbufu wowote.
Mmoja wa wapiga kura hao, Padre Francis Laswai ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari watakatifu Rufino na Rinaldo kutoka kijiji cha Kasumo Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma amesema amejitokeza kupiga kura baada ya kuona umuhimu wa kuchagua viongozi watakaowafaa.
Naye Abbas Rashid mkazi wa mtaa Mgera B kata ya Mwandiga Halmashauri ya Wilaya Kigoma amesema kuwa hadi kufikia mchana hakukuwa na tatizo lolote katika zoezi la upigaji kura tangu kufunguliwa mapema asubuhi ambapo kila mwananchi aliyefika kituoni alihudumiwa na kupata nafasi ya kupiga kura na watu wazima, wajawazito na wagonjwa walihudumiwa mapema na kuondoka.