RC Kigoma asifu uhusiano Tanzania, Burundi

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Burundi ni ishara ya ujirani mwema na undugu kati ya serikali na wananchi.

Andengeye amesema hayo leo wakati akifungua kikao cha pamoja cha Kamati ya Wataalamu (JTC) kati ya Tanzania na Burundi kinachoendelea mkoani Kigoma.

‘’Tunapaswa kusimamia uimarishaji mpaka baina ya nchi zetu ili kudumisha ushirikiano mwema na undugu,’’ amesema Andengenye

Advertisement

Amesema, Tanzania na Burundi zina mambo mengi ya ushirikiano ikiwemo nyanja za kibiashara, uwekezaji, uchumi na kidiplomasia hivyo uwepo kikao cha pamoja ni matokeo ya ushirikiano mzuri ambapo amewapongeza marais wa nchi hizo Rais Samia Suluhu Hassan, Evariste Ndayishimiye wa Burundi kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kudumisha ushirikiano.

Mkuu huyo wa mkoa amegusia pia suala la sekta ya usafirishaji ambapo ameweka wazi kuwa, sekta hiyo imeendelea kuimarika kutokana na ushirikiano wa nchi hizo mbili yakiwemo yale makubaliano ya mkakati wa ujenzi wa reli kutoka Uvinza- Kigoma hadi Msongati- Burundi.

Amesema, ujenzi wa reli hiyo mbali na mambo mengine utaufungua mkoa wa Kigoma sambamba na kuiwezesha Burundi kukuza uchumi wake kutokana na kurahisisha usafirishaji bidhaa jambo alilolieleza kuwa, litakuza sekta ya biashara, viwanda na uwekezaji kwa ujumla.

Kwa upande wake Kiongozi wa timu ya Wataalamu kutoka nchini Burundi, Meja Jenerali Mbonimpa Maurice amekielezea kikao hicho kuwa, utawawezesha wataalamu wa nchi hizo mbili kujadili kwa kina changamoto zilizojitokeza kwenye suala la mpaka wa kimataifa.

‘’Mipaka ipo lakini changamoto zinatokea hivyo tutakaa na kujadili changamoto hizi kwa lengo la kuimarisha mpaka wetu kwa manufaa ya nchi hizi mbili,’’ amesema Maurice.

Mkutano wa uimarishaji mpaka wa Kimataifa kati ya Tanzania na Burundi umeanza leo Novemba 18, 2024 na unatarajiwa kumalizika Novemba 22, 2024 ambapo mbali na mambo mengine wataalamu wanaoshiriki kikao hicho  watatembelea vijiji vya Bukililo na Nyakayenzi upande wa Tanzania na kijiji cha Kamusha nchini Burundi kwa lengo la kuangalia alama za mpaka.

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za afrika iwe imeimarishwa.