RC Mtwara aombwa ushirikiano changamoto za usalama
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara imeombwa kutoa ushirikiano na ufafanuzi kwa wawekezaji wa vivutio vya utalii hasa kwenye maeneo ya fukwe ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza hasa za usalama.
Hayo yamebainishwa wakati wa mwendelezo wa tamasha la Nyangumi mwaka 2024 linalofanyika kwenye viwanja vya Mashujaa Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwakilishi wa Meneja Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania, Deodat Mmanda amesema vipo visiwa viwili ambavyo bado havijapata wawekezaji kutokana na changamoto mbalimbali za kuwekeza kwenye hivyo visiwa ikiwemo sababu za kiusalama hali inayorudisha nyuma uwekezaji.
Aidha, metoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano na wafanye shughuli zao za uvuvi kwa kufuata utaratibu lakini pia kutofanya makazi kwenye maeneo ya visiwa kwani gharama kubwa inatumika kulinda hifadhi hizo kwa ajili ya kunufaika kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ameongeza kuwa Marine Park wako tayari kuimarisha miundombinu na kutatua changamoto ambazo zikifanyiwa kazi maeneo hayo yatakuwa bora zaidi na kuwahamasisha wananchi na taasisi mbalimbali kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo hayo ya hifadhi ili kuwavutia wageni.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo Wizara ya Maliasili na Utalii ambae pia ni mgeni rasmi wa tukio hilo, Dkt. Edward Kohi amesema wizara hiyo iko kwenye mpango wa kutembelea mkoa wa Mtwara na Lindi ili kuhakikisha vivutio vyote vilivyopo kwenye mikoa hiyo vinaingia kwenye mpango wa nchi.
Mpango huo ikiwa ni pamoja na kuvitangaza na kuviendeleza huku akiwaomba viongozi wa mikoa hiyo kutoa ushirikiano ili kuandaa mpango wa kuendeleza vivutio vilivyopo.
“Lengo la nchi na maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi mwaka 2025/2026 ni kuhakikisha kuwa wanafikia watalii milioni 5 hivyo ujio wa nyangumi utaongeza aina nyingine ya utalii na kuongeza idadi ya watalii”
“Kuwa na rasilimali ni kitu kimoja, kuvifanya kuwa kivutio cha watu ni ktu kingine hivyo wataalamu watakapo kuja muwape ushirikiano mkubwa ili tuweze kuandaa mpango wa kuviendeleza vivutio tulivyo navyo”amesema Kohi.
Amesema, wataalamu watakuja kuhakikisha zile rasilimali walizonazo zinabadilishwa kuwa vivutio na kufanya watu waweze kutembelea Mtwara pamoja na Lindi ili kuongeza idadi ya watalii wale wanaokuja tanzania waweze kuja na maeneo hayo.