RC Shinyanga aweka jiwe la msingi sekondari Bumva

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ameweka jiwe la msingi shule mpya ya sekondari Bumva, iliyopo kijiji cha Bumva kata ya Segese, Halmshauri ya Wilaya ya Msalala iliyojengwa kwa gharama ya Sh milioni 600.
Shule hiyo inatarajia kupokea wanafunzi zaidi ya 100 kutoka shule za sekondari ya Mwalimu Nyerere na Segese wanaotoka katika vijiji vya Bumva, Busongo C, Wisolele na Senta mashariki kwa vitongoji vya Misungwi na Itembe.

RC Anamringi amesema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha na kusogeza miundombinu ya elimu kwa wananchi kusudi kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata elimu na sio kuwatumikisha mashambani na kuchunga mifugo.

Katibu Tawala wa Mkoa, Salum Hamduni amesema serikali inayoongozwa imeendelea kutoa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ambapo zaidi ya Sh bilioni 6 zimetolewa kutekeleza miradi mbalimbali Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Rose Manumba amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo ikiwemo Shule ya Sekondari Bumva ambayo inakwenda kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu na utoro sugu.




