RUNGWE, Mbeya: WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx Gas Tanzania, leo Februari 08 inaendelea kusambaza mitungi ya gesi ya kilo sita kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya, uzinduzi rasmi umefanyika jana na kuanzia wilayani Rungwe.
Akiongea na msafara wa viongozi kutoka REA na kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited, asubuhi, kabla ya kuanza zoezi hilo, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mbeya, Said Maditto ameipongeza Serikali kupitia REA kwa kuanza rasmi zoezo hilo kwa kushirikiana na mtoa huduma kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited ambaye ameanza kugawa mitungi hiyo katika wilaya ya Rungwe, na wilaya zote ambapo Wananchi watanunua kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.

Maditto amesema kuwa mitungi ya gesi ambayo imeanza kusambazwa katika mkoa wa Mbeya itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi katika kupikia.
“Naipongeza REA kwa kuanza kutekeleza Mradi huu, nawapongeza pia kampuni ya Oryx Gas kwa kuwa, ina mtandao mkubwa wa utoaji wa huduma ya kujaza mitungi ya gesi hata baada ya kuisha, ombi langu tu Miradi kama hii iwe endelevu ili wananchi wengi, wafikiwe na nishati safi kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu,” amesema Maditto.
SOMA: REA yaendelea ilipoishia umeme nyumba kwa nyumba
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Nishati Safi mkoa wa Mbeya na Songwe kutoka REA, Venture Maganga amesema, serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya kusambaza nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji na kuwaomba Wananchi mkoani Mbeya kuchangamkia fursa ya kununua mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku ambayo ni Sh 20,000 tu kwa mtungi wa gesi wa kilo sita (6) na fedha inayobaki, inalipwa na Serikali.
“Lengo la sisi kuwa hapa ni kuzindua Mradi wa kuwezesha na Wananchi ili wapate huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti ovyo, ninawaomba Wananch wafike kwenye vituo wakiwa na Vitambulisho vya NIDA kwa ajili kununua mitungi hii pamoja na vifaa vyake kwa bei ya ruzuku ya Sh 20,000,” ameongeza Maganga.

Naye, Alex Wambi, Meneja Mauzo wa Oryx Gas Tanzania Bara ametoa wito kwa Wananchi kufika kwenye vituo vya mauzo ili kununua mitungi hiyo ya gesi na kuongeza kuwa maandalizi yote yamefanyika ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma kwa wakati na bila usumbufu wowote.
Maganga amezitaja wilaya zitakazonufaika na mgao wa majiko hayo kwa mkoa wa Mbeya kuwa ni wilaya ya Rungwe, Chunya, Kyela, Mbarali na Mbeya.