Katika jua la asubuhi lenye mng’ao wa dhahabu, wafanyakazi wa Redio Ebony FM ya mjini Iringa, walikusanyika pamoja na watoto walio katika mazingira magumu.
Siku hii ya leo, Februari 14, siku ya wapendanao, imekuwa tofauti kwa Redio Ebony FM kuitumia—kuwapa watoto hawa upendo na faraja waliyoikosa kwa muda mrefu.
Baadhi ya watoto hao walipelekwa River Valley Campsite, eneo safi. Hapo watoto walipewa nafasi ya kusahau changamoto zao na kufurahia siku iliyopambwa na michezo, muziki, na chakula cha pamoja na wafanyakazi wa Redio Ebony FM.
Nancy Mfugale, Mkurugenzi wa Redio Ebony, alisimama mbele ya hadhira iliyojumuisha watoto na wageni waalikwa na kueleza kwa nini walichagua kufanya tukio hili maalum.
“Tuliposikia na kuripoti matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto, tuligundua kuwa hatuwezi kubaki kimya. Tuliamua kupaza sauti, na baada ya miezi miwili ya maandalizi, leo tumekuja hapa kuwapa watoto hawa upendo na matumaini,” alisema kwa msisitizo.
Mtazamo wake ulithibitishwa na Leonard Mgina, mwanasaikolojia aliyeshiriki katika tukio hilo. Alieleza jinsi kukosekana kwa malezi bora kunavyochangia ongezeko la watoto wa mitaani.
“Tunaposhindwa kuwajibika kama jamii, tunawasukuma watoto hawa katika mazingira hatarishi. Kupitia programu ya Ebony FM ya Gusa 2025 – Sisi ni Familia, tumeona jinsi elimu inavyoweza kusaidia kupunguza migogoro ya kifamilia na kurudisha maadili katika jamii,” alisema.
Athari za ukosefu wa malezi bora zilielezwa kwa kina na mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP George Buzema.
“Mtoto asipopata huduma bora, tunamuweka katika hatari ya kuwa mhalifu wa kesho. Kupitia dawati la jinsia na watoto, tumejitahidi kuwafikia watoto waliopo katika mazingira magumu na kuwaelimisha wazazi na walezi kuhusu wajibu wao,” alisema.
Mwakilishi wa Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Lenatus Mwangeni, aliongeza kuwa elimu kuhusu ukatili dhidi ya watoto ni muhimu kwa kila mzazi na mlezi.
“Wazazi wanapaswa kuelewa kuwa mtoto hapaswi kuonywa kwa kupigwa. Tunatoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto wanaokumbwa na ukatili na kuwaelimisha wazazi juu ya njia bora za malezi,” alieleza.
Mbali na hotuba hizo, watoto walishiriki michezo mbalimbali, walicheza muziki, na wakapata fursa ya kuzungumza na watu waliokuja kuwaunga mkono.
Furaha ilionekana wazi usoni mwao, ikidhihirisha kuwa, kwao, siku hii ilikuwa ya kipekee. Katika hotuba yake, Nancy Mfugale alisisitiza kuwa upendo kwa watoto haupaswi kuwa wa siku moja pekee.
“Hawa ni watoto wetu kama watoto wengine. Leo ni siku ya upendo, lakini tusisahau kuwa wanahitaji malezi na faraja kila siku. Huu ni mwanzo wa safari ndefu ya kuhakikisha kuwa watoto hawa wanapata haki zao na wanakuwa viongozi wa kesho,” alisema.
Siku hiyo ilimalizika kwa watoto kushikana mikono na kuimba wimbo wa matumaini. Ingawa walirejea katika vituo vyao jioni, mioyo yao ilikuwa imetawaliwa na faraja, upendo, na ndoto mpya za maisha yenye matumaini.
Howdy! Someone in my Myspace group shared this website with us so I came to give it a look.
I’m definitely enjoying the information. I’m book-marking and will be tweeting this to my followers!
Excellent blog and amazing design.