Ripoti ya Jaji Chande yatajwa kufichua mambo matano makubwa

IRINGA: Ripoti ya Tume iliyoongozwa na Jaji Mohamed Chande Othman imeendelea kuzua mjadala mkubwa nchini, huku mchambuzi wa masuala ya uongozi, uchumi na siasa Tanzania, Dk Netho Ndilito (PhD), akiitaja kuwa nyaraka muhimu iliyofichua mambo makubwa matano yenye maslahi kwa taifa.
Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, mchambuzi wa siasa, Dk Ndilito alisema baada ya kupitia maoni ya Watanzania, wanamitandao na wachambuzi mbalimbali, amebaini kuwa taarifa hiyo imeleta mwanga mpya kuhusu hali halisi ya taifa na changamoto zilizokuwa zikijadiliwa kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Dk Ndilito, jambo la kwanza ni kwamba ripoti hiyo imeliponya taifa kwa kueleza ukweli ambao kwa muda mrefu haukupata nafasi ya kujadiliwa waziwazi.
Alisema jambo la pili lililobainishwa ni kufichuliwa kwa nia na dhamira ovu za baadhi ya watu waliotamani vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, jambo ambalo sasa limewekwa wazi kupitia uchunguzi huo.
Aidha, alieleza kuwa ripoti hiyo imeweka bayana upotoshaji na taarifa zisizo sahihi zilizokuwa zikisambazwa na baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa, huku wakitamani kuona nchi ikiingia kwenye machafuko.
Katika hoja ya nne, Dk Ndilito alisema ripoti hiyo imeonesha namna Watanzania wengi wanavyoipenda nchi yao, kuiamini serikali yao na kutokuwa tayari kushawishika kuivuruga amani, umoja na mshikamano wa taifa.
Jambo la tano alilotaja ni kwamba taarifa hiyo imeonesha uimara wa serikali pamoja na ukomavu wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kushughulikia masuala ya ndani kwa weledi na utulivu.
Dk Ndilito alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kuendelea kudumisha umoja, upendo, mshikamano na amani, akisisitiza kuwa huo ndiyo utamaduni uliojenga heshima ya taifa kwa miaka mingi.
“Watanzania wameendelea kuonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na uzalendo. Hii ndiyo desturi yetu kama taifa,” alisema.



