Royal Tour inavyoakisi utalii wa Tanzania kimataifa

MWAKA 2022 wakati wa uzinduzi wa filamu ya Tanzania, The Royal Tour jijini Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan alisema, “Tangu kutengenezwa kwa fi lamu hii Sekta ya utalii imeanza kukua tena baada ya wadau wengi duniani kutuunga mkono.”

“Ni ushauri wangu sasa na sisi kama taifa tuanze kujipanga kwa kufanya marekebisho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuangalia ubora wa hoteli zetu, magari yanayobeba watalii, miundo mbinu ya viwanja vya ndege, namna tunavyowahudumia wageni wetu katika maeneo mbalimbali na mengine mengi ili ule ukarimu niliokuwa nikiusema wakati tunatengeneza filamu hii uonekane kwa vitendo.”

Haya yanadhihirisha hali halisi iliyopo katika Maonesho ya Dunia ya Utalii na Biashara ya EXPO 2025 yanayoendelea katika jiji la Osaka Kansai nchini Japan.

SOMA: Filamu ya “The Royal Tour” yazaa matunda

Kwa mujibu wa Tovuti ya Wizara ya Biashara na Viwanda iliyotolewa jijini Dodoma Aprili 8, 2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo Tanzania inatarajiwa kushiriki maonesho hayo yanayofanyika Osaka, Japan Aprili 12 hadi 13 Oktoba, 2025. Maonesho hayo yatashirikisha nchi 160 na yanatarajiwa kuwa na watembeleaji zaidi ya milioni 28.2.

Kwa mujibu wa Jafo, Siku ya Kitaifa ya Tanzania ni mojawapo ya matukio makubwa yanayoratibwa yatakayofanyika Mei 25,2025. “Nchi (Tanzania) itatumia siku hiyo kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji, vivutio vya utalii pamoja na mila na utamaduni wa Kitanzania ambapo mgeni rasmi katika maonesho ya Expo 2025 Osaka, ni Waziri Mkuu Kasim Majaliwa,” inasema taarifa katika tovuti hiyo.

Katika maonesho hayo, kila mgeni anayetembelea banda la Tanzania anazungumzia namna alivyofahamu rasilimali zilizopo baada ya kuangalia filamu hiyo. Uzuri na sifa za Tanzania unalifanya banda la Tanzania katika maonesho hayo kuwa na harakati nyingi za wageni.

Wengi wanafika kutaka kupata maelezo ya kina kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, ukarimu wa watu wake na namna watakavyoweza kufunga safari na kwenda kuona yanayoelezwa kupitia Filamu ya ‘Royal Tour’ na ile ya ‘Amaizing Tanzania’ ambazo zinaoneshwa katika maonesho hayo.

“Najitahidi kupambana ili baada ya EXPO mwaka huu nikifunga ndoa, nije Tanzania na mke wangu kwa ajili ya mapumziko ya harusi.” “Niliona Royal Tour iliyofanywa na Rais wenu (Samia) na hapa nimepata maelezo mengi yanayonifanya niichague nchi yenu kwa ajili ya mapumziko,” anasema Turuke Nioko raia wa Japan aliyefika katika banda la Tanzania.

Mawazo ya Mjapan huyo yamebeba hisia za wananchi wengi katika taifa hilo pamoja na mataifa mengine waliotembelea EXPO 2025. Inakadiriwa kuwa hadi kumalizika kwa maonesho hayo, zaidi ya watu milioni 30 duniani watakuwa wameyatembelea na kujifunza mengi kuhusu uzuri wa Tanzania.

Meneja wa Banda la Tanzania katika maonesho hayo, Deo Shayo anasema: “Kazi iliyofanywa na Rais Samia kuifungua Tanzania katika sekta ya utalii kwa kweli inaonekana katika maonesho haya.” “Ni matarajio yetu Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake itajitahidi kuhakikisha wadau wa utalii katika maonesho haya wanaendelea kuwepo ili kujibu hoja mbalimbali kutoka kwa wageni wetu.”

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ambao ndiye msimamizi mkubwa wa maonesho hayo, vivutio kama Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Serengeti, Ziwa Manyara na Visiwa vya Zanzibar vimeongoza kwa kupata watembeleaji wengi kutaka kujua taarifa zake.

“Wengi wa wageni wetu hapa wanataka kujua kuhusu vivutio hivyo, ndiyo maana tunatamani kuona wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiendelea kuwepo katika banda letu kwani uwepo wao umeleta hamasa kubwa kwa watembeleaji, tumeweka picha ya Rais Samia pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro na baadhi ya watembeleaji wamekuwa wakitumia eneo hili kupiga picha huku wakisema wamependa sana filamu yake ya Royal Tour,” anasema Shayo.

Anasema watembeleaji wengi wa banda hilo walikuwa wakifika moja kwa moja na kuanza kuuliza habari za vivutio vya Tanzania na kueleza wazi kwamba filamu hiyo imewasukuma kulitafuta banda la Tanzania. Mmoja wa raia wa Ufaransa, Lucie Bernade anasema: “Nimeona kwenye The Royal Tour mambo mengi mnayoeleza hapa, natamani siku moja ndoto zangu zitimie nije kuona mwenyewe vile ambavyo nimeviona kwenye filamu ile.”

“Kwa kweli Rais wenu amefanya kazi kubwa kwani ukiiangalia ile filamu unahamasika kutaka kufika Tanzania na kujionea kwa macho, inaonekana ni nchi nzuri sana.”

Akizungumzia kutambulika kwa Tanzania na sura nzuri ya nchi hiyo kwa wageni wengi Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda anasema juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kukuza na kutangaza utalii pamoja na maendeleo yaliyopatikana yamesababisha watu wengi kuwa na ufahamu mkubwa wa vivutio vilivyopo Tanzania.

Anasema kazi kubwa inayotakiwa kufanyika sasa ni watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuboresha huduma za utalii katika kila eneo. “Tunapata sifa kubwa kimataifa, ni matumaini yetu kama taifa sasa kila mmoja wetu kujifunga mkaja kuhakikisha katika kila sekta tunatoa huduma nzuri ili kazi kubwa iliyofanyika ya kuitangaza nchi yetu iweze kuwa na tija na hivyo kuongeza idadi ya watalii.”

“Hapa Japan wenzetu wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa hivyo na sisi kwa jitihada hizi nina imani tutafanikiwa.” anasema Balozi Luvanda.

Kauli ya balozi huyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ernest Mwamwaja anayesema jitihada zinafanyika kwa kiasi kikubwa kushirikisha kila taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kuwa huduma za utalii nchini zinakuwa bora zaidi kuunga mkono kwa vitendo kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia.

“Tumejipanga vizuri na tunaendelea kujipanga kuhakikisha miundombinu ya utalii kama vile barabara za kuwafikisha watu kwenye hifadhi, sehemu za kulala wageni, magari na miundombinu mingine inakuwa imara ili wageni hawa wanaoonesha nia ya kutembelea nchi yetu wakifika wavutiwe zaidi na kurudi tena, lakini wao pia wawe mabalozi wetu wazuri kuitangaza sekta ya utalii,” anasema Mwamwaja.

Anaongrza: “Kwa niliyoshuhudia kwenye EXPO 2025 Japan, Rais Samia ametengeneza njia ambayo bila shaka wadau katika sekta ya utalii wakiifuata na kuzingatia maono yake, idadi ya watalii nchini itaongezeka kadri miaka inavyokwenda na kuifanya sekta hiyo kuendelea kung’ara kimataifa.”

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, katika miaka minne iliyopita Tanzania imepata wageni zaidi ya milioni tano waliotembeela vivutio vya utalii. Kwa msing huo ni dhahiri kuwa, kuendelea kushiriki katika maonesho na misafara ya utalii kutoka Ulaya, Asia na nchini Marekani kutaendelea kuongeza idadi kubwa zaidi ya watalii kutoka nje.

 

 

Mwandishi ni Kaimu Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya EnWeo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button