Rufaa 28 za watumishi wa umma zakataliwa
TUME ya Utumishi wa Umma (TUU) imepitia, kujadili na kuamua rufaa na malalamiko 88 huku rufaa 28 kati ya 63 za watumishi wa umma zikikataliwa.
Aidha, kati ya rufaa zilizoamuliwa, makosa yaliyoonekana kutendwa zaidi ni utoro kazini, wizi wa mali za umma, rushwa na kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo, Kaimu Katibu wa tume, John Mbisso alisema uamuzi umefikiwa katika mkutano wa pili kwa mwaka 2025/26 uliofanyika Desemba Mosi hadi 19, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu, Hamisa Kalombola.
Alisema kati ya rufaa na malalamiko hayo, rufaa zilikuwa 63 na malalamiko ni 25.
SOMA: Watumishi wa umma waonywa dharau, maringo
Mbisso alifafanua kuwa upande wa rufaa 63 zilizoamuliwa na tume, 15 zilikubaliwa bila masharti na 14 zilikubaliwa kwa masharti kwamba mamlaka za nidhamu kuanza michakato upya.
Alisema pia rufaa 28 zilikataliwa, sita zilitupiliwa mbali baada ya kuwasilishwa nje ya muda unaotakiwa kisheria wa siku 45 kuwasilisha rufaa zao.
Kwa upande wa malalamiko, Mbisso alisema kati ya malalamiko 25 ambayo tume imeyatolea uamuzi, 13 yalikubaliwa, sita yamekataliwa, sita yalitupiliwa mbali kutokana na kuwasilishwa nje ya muda.
Alisema katika rufaa zilizowasilishwa na kuamuliwa, makosa yaliyoonekana kutendwa zaidi na watumishi wa umma ni utoro kazini, wizi wa mali za umma, rushwa, kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo.
Pia, kukiuka maadili ya utumishi wa umma, uzembe uliosababisha hasara kwa serikali na uzembe wa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo.
Mbisso alisema kwa upande wa malalamiko yaliyowasilishwa na kuamuliwa na tume yalihusu kupinga watumishi kutolipwa stahili zao na waajiri wao ikiwemo mishahara, stahili za uhamisho na posho za kisheria zinazotokana na kutekeleza majukumu yao.
Pia, kuondolewa kwenye utumishi wa umma kinyume na sheria na kusitishwa kwa ajira kinyume na sheria.
Alisema warufani 24 na warufaniwa wanne waliomba na kuruhusiwa kufika mbele ya tume kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao za rufaa zilizowasilishwa kwa tume ikiwa ni kwa mujibu wa Kanuni ya 62 (1) ya Kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022.
Alisema pia mamlaka za nidhamu tano ziliitwa mbele ya tume kwa ajili ya kutoa maelezo kutokana na kutotekeleza maagizo ya tume yaliyotolewa katika mikutano iliyopita.
Tume ilipitia taarifa za utekelezaji wa majukumu katika robo ya kwanza kwa mwaka 2025/2026.
Aidha, Mbisso alisema katika kutekeleza jukumu la urekebu, tume ilifanya ziara za kikazi katika taasisi za serikali tano.
Nazo ni Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI).
“Lengo la ziara hizo lilikuwa ni kutoa elimu kwa waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu kuhusu uzingatiaji sheria, kanuni na taratibu katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimali watu,”alisema.



