DAR ES SALAAM; TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeagiza watumishi wa umma wazingatie maadili na misingi ya haki za binadamu wanapohudumia wananchi na waache maringo na kejeli.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu alisema mtumishi wa umma akienda kinyume na taratibu vikiwemo vitendo vya rushwa au kukiuka haki za binadamu ni tusi kwa kiongozi wa serikali, hivyo hastahili kuonewa huruma.
Jaji Mwaimu alisema hayo Dodoma jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa 2024 ambayo yaliadhimishwa kwa kongamano la watumishi wa umma.
“Mtumishi wa umma anapotoa huduma kwa upendeleo, dharau, dhihaka, chuki maringo na kejeri anakuwa amekiuka baadhi ya kanuni hizo. Hivyo tuzingatie maadili katika kutekeleza majukumu na tuwajibike kwa tunaowahudumia kwa kuzingatia takwa la Katiba inayosema Serikali itawajibika kwa wananchi,” alisema.
Aliongeza: “Mtumishi wa umma akienda kinyume na taratibu zilizowekwa, ikiwa ni pamoja na kujihusisha na vitendo vya rushwa au kukiuka haki za binadamu ni tusi kwa kiongozi wa serikali, hivyo hastahili kuonewa huruma”.
Jaji Mwaimu alisema ukuzaji, ulinzi na kuheshimu haki za binadamu ni nguzo muhimu katika utawala wa nchi kama ilivyoelezwa kwenye Katiba na Tamko la Haki za Binadamu.
Alisema watumishi wa umma wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na kuwa ndio msingi wa amani na umoja kuzidi kuimarika na kuendelea kudumu.
“Nchi yenye umoja na amani ni rahisi kuleta maendeleo haraka kwa kila mtanzania na nchi kiujumla,” alisema.
Aliwataka pia watumishi wa umma ambao ndio injini kutumia falsafa ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuzingatia maadili na haki za binadamu.
Jaji Mwaimu alisema watumishi wa umma ni chachu ya maendeleo, usalama, umoja na mshikamano wa nchi kwa kuwa wanasimamia sheria, kanuni na miongozo.
Aliwahakikishia watumishi wenye ubinafsi na wasiozingatia maadili na haki za binadamu kuwa vyombo vya kuchukua hatua vipo.
Aliwaagiza watumishi wa umma waache kufanya kazi kwa mazoea na kuwa anataka kuona hatua zinachukuliwa dhidi ya watumishi wa umma wanaokwamisha maendeleo kwa kutozingatia maadili na haki za binadamu.
“Hivyo nawasihi tujitathmini, tuheshimu Katiba, sera na sheria za nchi na tuungane kama watumishi wa umma katika kuleta maendeleo na kudumisha amani nchini,” alisema Jaji Mwaimu.
Alisema kupitia vyombo vya habari kumekuwa na malalamiko ya wagombea kuenguliwa na changamoto zinginezo zilizojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Sisi kama watendaji baadhi yetu tulisimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, tusipuuze malalamiko hayo ambayo wengine walijitokeza hadharani na tunapaswa kutafakari na kuyafanyia kazi ili changamoto hizo zisijitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” alisema Jaji Mwaimu.