Rufaa mgogoro madini ya Tanzanite yatupiliwa mbali

RUFAA ya kupinga maamuzi ya kamati juu ya mgogoro wa uchimbaji kati ya mgodi wa Kampuni ya Gem & Rock Venture uliopo kitalu B na Kampuni ya Franone inayomiliki mgodi wa kitalu C na serikali iliyokatwa na Gem & Rock Venture kwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini imetupiliwa mbali.

Kampuni hiyo imeamuriwa kufuata maamuzi na masharti ya kamati yaliyotolewa Machi 28 mwaka huu na sio vinginevyo.

Taarifa Ofisa Mfawidhi wa Madini Mirerani ,Mernad Msengi ilisema kuwa Machi 13 mwaka huu wachimbaji wa mgodi wa Gem & Rock Venture wakiongozwa na Mkurugenzi wake Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti walivamia mgodi wa Franone uliopo kitalu C zaidi ya mita 650 na kufanikiwa kuchimba na kupata madini ya Tanzanite kilo 4 na kuwashambulia na kuwajeruhi viongozi wa taasisi za ulinzi za serikali ndani ya mgodi huo.

Baada ya tukio hilo serikali iliamua kuufunga mgodi huo baada ya kamati ya watu watatu ambao ni wataalamu wa mipaka na miamba mgodini kutoka Dodoma kubaini kuwa Saitoti na wafanyakazi wake walichimba kinyemela madini ndani ya Kitalu C kinachomilikiwa na Mwekezaji Mzawa Onesmo Mbise kwa kushirikiana na serikali.

Saitoti alipinga maamuzi ya kamati hiyo na alikata rufaa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na kudai kuwa maamuzi ya kamati hiyo hayakuzingatia sheria na kanuni za madini hatua ambayo imepingwa vikali na Katibu Mkuu Wizara ya Madini.

Katika nakala ya barua aliyoandikiwa Saitoti na Katibu Mkuu Wizara ya Madini iliyoisaini na Kamishina wa madini, Dk Ibdullahaman Mwanga ilimwelekeza Saitoti mambo manne ya kutekeleza ikiwa ni pamoja na kurudi katika eneo la mgodi wake kama leseni inavyomwelekeza kwa kuwa alikuwa akichimba nje ya mgodi na kinyume na leseni aliyopewa.

Nakala ya barua hiyo ya Mei 17 mwaka huu ilimwelekeza kusimamisha shughuli za uchimbaji madini kwa kusisitiza nakala ya barua ya march 14 mwaka huu pamoja na hati ya makosa iliyotolewa march 16 mwaka ya kumtaka aweke geti na ukuta katika mgodi wake kutengenisha mgodi wake na kitalu C.

Hata hivyo Saitoti hakuweza kupatikana kueleza kama amekubaliana maamuzi ya rufaa yake au la kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa.

Habari Zifananazo

Back to top button