Rushwa ya ngono isiruhusiwe kutesa wanawake katika uchaguzi

BADO takribani miezi minne Watanzania wakutane katika vituo vya kupigia kura kufaidi uhondo wa demokrasia katika mfumo wa siasa za vyama vingi uliorejea nchini mwaka 1992 na uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo huo kufanyika Oktoba 1995.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kila mwenye sifa ana haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu ama iwe kwa kuwania kugombea ili achaguliwe, au kwa kuchagua wengine, mradi tu uchaguzi ni haki ya kidemokrasia yenye taratibu zake.
INEC inasema miongoni mwa sifa za mtu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi huu ni kwanza, awe Mtanzania mwenye umri usiopungua miaka 18, mwenye akili timamu na aliyejiandikisha au kurekebisha taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kazi hii kwa awamu ya pili, imekamilika takribani wiki moja hivi iliyopita. Kuhusu kugombea, mhusika lazima awe mwanachama wa chama cha siasa chenye usajili wa kudumu ama awe mwanaume, au mwanamke. Kila mmoja ana nafasi na haki sawa na mwenzake.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali wakiwamo watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia, wanawake na wanaume wana uwezo wa kuongoza.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani aliwahi kunukuliwa akisema, kama ilivyo kwamba wapo wanaume wasioweza kuongoza, ndivyo ilivyo kwamba wapo wanawake wenye uwezo mkubwa wa kiuongozi. Mifano halisi ni uwezo mkubwa anaouonesha Rais Samia Suluhu Hassan katika uongozi,
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson pamoja na imani juu ya uwezo wa Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah hadi kuchaguliwa hivi karibuni kuongoza nchi hiyo.
Hata hivyo licha ya ukweli huu kufahamika, bado wanawake wengi hawajisikii kujitokeza kuwania nafasi za uongozi hususani wa kisiasa kutokana na sababu mbalimbali hasa kero ya rushwa ya ngono ambayo ni mada ya makala hii.
Katika moja ya mikutano na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben anasema, “Rushwa ya ngono ipo, lakini haizungumzwi maana inachukuliwa kama jambo la kawaida na lisilozungumzwa hadharani…”
Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007, Kifungu cha 25, mtu yeyote anayebainika kutumia mamlaka ya utekelezaji majukumu yake kuomba au kutoa upendeleo wa kingono, kama kigezo cha kutoa ajira, kupandisha cheo, kutoa haki au huduma, atashitakiwa chini ya Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi.
Sheria hiyo inasema mtu huyo akitiwa hatiani, anaweza kuhukumiwa faini isiyozidi Sh milioni tano, au kifungo cha miaka 20 jela, au adhabu zote kwa pamoja. Watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia pamoja na wadau katika mapambano dhidi ya janga la rushwa hasa ya ngono wanasema waathirika wakubwa wa rushwa hii ni wanawake.
Kimsingi, rushwa ya ngono kama aina ya rushwa inayoathiri siasa na uchaguzi, huathiri ushiriki wa wanawake katika mchakato wa siasa na uongozi. Hii ni kwa kuwa inapoachwa wazi na mlengwa mwenyewe kukosa msimamo ukiungwa mkono na jamii, humfanya mwanamke katika mchakato wa uchaguzi kuzungukwa na ‘mafisi wa ngono’.
Sumu ya rushwa ya ngono hufufuka zaidi katika kipindi cha vyama kuteua wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali.
Uchunguzi wa gazeti la HabariLEO unabaini kuwa, hufanywa pia na wapambe wa wenye mamlaka sambamba na wanaojidai ni magwiji wa kampeni, wakiwamo baadhi ya wanaotaka kunadi wagombea. Wanachosema wengi ni kuwa, wanawake wana uwezo mkubwa kiuongozi, waachwe washiriki mchakato ili jamii ipate viongozi bora bila kujali ni mwanamke au ni mwanaume.
Waachiwe mazingira rafiki watumie uwezo wao kujinadi, kuchaguliwa na kutumikia jamii. Ni dhahiri kuwa, wapo wanawake wengi ‘wanaojua siasa’ na wenye uwezo wa kisiasa, lakini hawajashindana kwa kuwa, ama hawana rasilimali za kutosha kupambana, au wanaogopa kero zinazoweza kujitokeza mbele yao, ikiwamo ya kudaiwa rushwa ya ngono.
Chapisho moja mtandaoni limeandika likisema miongoni mwa mambo yanayofanya gonjwa hili liendelee kuwapo ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria zinazozuia na kupambana na rushwa ya ngono hivyo, hawafahamu haki zao inapotokea wanaombwa rushwa hiyo.
Nyingine vyanzo vinasema ni watendewa kuogopa kutoa taarifa kwa kuhofia kusimangwa, kubezwa, kufanyiwa kejeli, kunyanyapaliwa na hata kunyimwa huduma.
Hata hivyo, suala la rushwa ya ngono ni gumu kuthibitisha kwa kuwa hufanyika kwa usiri. Kwa msingi huo, toa
ushirikiano na vyombo husika wakati wa uchunguzi na kutoa ushahidi.
Mtu anapodaiwa rushwa ya ngono ili apitishwe kugombea nafasi au apewe madaraka yakiwamo ya kiuteuzi, ashirikishe vyombo husika hasa kwa kutoa taarifa mapema na kutoa ushahidi ili wahusika waadhibiwe kisheria.
Mwenyekiti mstaafu wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA – TAN), Salome Kitomari anasema silaha imara dhidi ya rushwa ya ngono ni kila mmoja kujitambua na kujiongeza thamani kwa kutokuwa tegemezi ili kutofungua milango ya watu kujaribu kumtumia kama chombo cha starehe.
Mchungaji Kiongozi wa Ebenezer Gospel Church (Kisima cha Uzima), Kijichi Dar es Salaam, Kizitto Noya anasema, “Kudai rushwa ya ngono ni kosa linawagharimu na kuwaathiri wahusika kiroho kwa kuwa wanachafua Hekalu la Mungu (miili yao) kwa uzinzi na uasherati ambao ni dhambi ya kujitakia na rahisi kuepuka.”
Kizitto anaongeza kuwa, “Hakuna mtu mwenye mamlaka yoyote katika jambo au taasisi yoyote hivyo, ukiona unaingia katika hatari ya kuombwa rushwa ya ngono na mfumo wa ndani haukusaidii, tafuta msaada nje. “Toa taarifa kwenye vyombo vingine hatua zichuliwe haraka ili uwe salama. Usiogope maneno ya watu kwa kuwa ni haki na wajibu wako kudai na kutafuta haki yako ya kuwa salama…”
Hata hivyo ukweli ni kwamba, licha ya ugumu huo, wanawake wengi ni imara na wasioyumbishwa maana hata wakiombwa rushwa hiyo, hawatoi badala yake, wanaendelea na mapambano hatimaye, wanashinda na kuwa viongozi bora.
Kwa msingi huo, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), vyombo vya dola na wadau wengine waweke mkazo katika elimu kuhusu rushwa zote wakati wa uchaguzi na hasa rushwa ya ngono.
Nguvu kubwa iwekwe kwa wanasiasa chipukizi ili wawe na ‘macho ya kuona’ na ‘masikio ya kusikia’ ‘lugha na sura’ za rushwa, ikiwamo rushwa ya ngono. Kila mmoja ajue kuwa utu wake na wa mwingine una thamani kubwa inayopaswa kulindwwa kila wakati, kila mahali, kila namna na kila mtu.
Ili kupambana vizuri dhidi ya rushwa, wanaobainika kuhusika wachukuliwe hatua kali, ikiwamo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria huku mashuhuda wakitoa ushirikiano wa ushahidi kuwatia hatiani wahusika vinginevyo, waovu wa namna hiyo watazidi kuongezeka.
Ijulikane wazi na mapema kuwa, kiongozi anayepatikana kupitia rushwa ya ngono huwa mzigo katika nafasi yake na daima ataongozwa kupitia akili za wengine.



