WAKATI Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, wadau wa masuala ya jinsia wamewataka wanaume mahala pa kazi kukagua vyeti na si maungo.
Hayo yamesemwa leo Novemba 29, 2022 na Mwakilishi wa Mtandao wa Ushirikishaji Wanaume ‘Men Engage’ Dk Katanta Simwanza ambaye amesema wanaume hawana budi kuwa sehemu ya mapambano hayo kwa kuwa wao ndiyo wafanyaji wa vitendo hivyo
“Wanaume tunapaswa kujua kwamba rushwa ya ngono inaathiri utendaji na hata kuua ndoto za wanawake wengi, hebu kazi yetu iwe kukagua vyeti na sio maungo,”amesema Dk Simwanza.
Nae, Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili wa kijinsia (Mkuki) wakili Anna Kulaya amesema Serikali iharakishe kuridhia mkataba wa kimataifa unaopinga rushwa ya ngono mahala pa kazi kwa kuwa utasaidia kuweka msimamo wa serikali dhidi ya vitendo hivyo na kufikia ziro ifikapo 2030.
“Lengo ni kuhakikisha Tanzania inafikia ziro katika ukatili wa kijinsia, ziro katika ukeketaji na ziro katika ndoa za utotoni na hilo linawezekana tukiunganisha nguvu ya pamoja.” Amesema Kulaya na kuongeza
“Huu mkataba sio mbaya na hauna athari yoyote kwetu ndiyo maana tunaomba Serikali iuridhie ili tuwe na njia na mwongozo wa pamoja wa kukabiliana na changamoto hii,” amesema Anna na kuongeza
“Tunaiomba Serikali kuharakisha kuridhia mkataba wa namba C 190, hii itasaidia katika kupambana na vitendo vya rushwa ya ngono na unyanyasaji mahala pa kazi.” Amesisitiza
Amesema Mtandao wa Mkuki umehakikisha kunaanzishwa Madawati ya Kijinsia vyuoni ili kusadia mapambano dhidi ya vitendo vya Rushwa ya Ngono hata hivyo, ni vyuo 20 tu ndio vimeanzisha madawati hayo.
“Sote tuna wajibu wa kuwa mstari wa mbele na kuhakikisha tunapinga vitendo vya Rushwa ya Ngono vyuoni na pahala pa kazi, Waziri Mkuu mwaka jana Novemba 25, alizindua muongozo wa Dawati la Jinsia katika taasisi za Elimu, na alisisitiza shule zenye wanafunzi wa jinsia zote ziwe na walimu wa jinsia zote na si jinsia moja, pia utekelezaji wa mwongozo huo usiishie katika taasisi za juu tu, bali ufike hadi katika shule za Msingi..
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben kwa upande wake amesema licha ya kelele nyingi kupigwa na wadau mbali mbali wa asasi za bado maeneo mengi ya kutoa huduma za kijamii ikiwemo mahala pa kazi na vyuoni, rushwa ya ngono inaendelea kukuwa siku hadi siku.
Amesema kupitia tafiti na miradi mbalimbali iliyofanywa na chama hicho imebaini kuwa rushwa ya ngono imechukua hatamu sehemu za kazi na kwenye taasisi za elimu ya juu.
Hata hivyo Dk Rose amebainisha kuwa changamoto kubwa ni ukimya dhidi ya vitendo hivyo hali inayosababisha kuendelea kufanyika kwa siri na kuathiri wengi.
“Tulifanya utafiti kuangalia rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari, na vyuoni tukabaini huko hali ni mbaya na bahati mbaya ni kwamba hawazungumzi. Kati ya waliohojiwa asilimia 52 hawakuwa wazi kusema kuhusu hilo, ni asilimia 48 tu ndio wameweza kusema” amesema Dk Rose.