Ruto ataka Bunge kutafakari hoja za Raila

RAIS William Ruto wa Kenya ameanza kushughulikia madai ya kinara wa upinzani, Raila Odinga na hali hiyo imefanya kusitishwa kwa maandamano yanayoongozwa na Raila aliyesema wako tayari kushiriki mchakato.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mawasiliano Ikulu, Emmanuel Talam, jana Ruto alikutana na viongozi wote wakuu wa Bunge na kupendekeza kupatikana mtazamo wa pande mbili kuhusu masuala aliyoibua Raila na kuitisha maandamano.

“Rais amefanya mkutano na uongozi wa Bunge ili kuunda mfumo kujadili namna ya kushughulikia hoja zilizotolewa na upande wa upinzani,” alisema Talam.

Katika hotuba yake ya kitaifa Ikulu, Ruto amenukuliwa akisema: “Ninamsihi kaka yangu Raila Odinga na upinzani, kusitisha maandamano na kutoa nafasi kwa mtazamo wa pande zote mbili ili tuipeleke nchi mbele.”

Aliongeza: “Wakati huo huo, ninatoa mwito kwa Wakenya wote kuwa watulivu na watiifu wa sheria na ninawahakikishia kuwa Serikali ya Kenya itaendelea na jukumu lake la kulinda maisha na mali zao ikiwa ni pamoja na biashara zao.”

Kwa upande wake, Raila alisema wameamua kusitisha maandamano ya Jumatatu na Alhamisi ili kuruhusu mazungumzo kuhusu masuala waliyoyaibua likiwamo suala la ugumu wa maisha kwa wananchi wa Kenya.

“Tuko tayari kushiriki na tutajihusisha bila aina yoyote ya vikwazo na mchakato huu unapaswa kuanza mapema kesho,” alisema Raila aliyeshindwa na Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti mwaka jana.

Raila na viongozi wa Azimio waliibua masuala mazito ikiwa ni pamoja na kulalamikia gharama ya maisha na suala la uteuzi wa makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mahakama ya Juu ya Kenya ilipitisha kwa kauli moja matokeo ya uchaguzi wa Agosti yaliyomtangaza Dk Ruto kuwa Rais lakini, Raila anapinga na kukataa kumtambua Ruto au serikali yake.

Ruto alisema Kamati ya Bunge ya pande mbili inaweza kuchunguza uwezekano wa mageuzi ya utaratibu wa uchaguzi, na akamtaka Raila kutumia vema fursa hii.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button