MKUU wa Mkoa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amesema mkoa huo una akiba ya chakula kutosheleza wananchi wake na kwamba kwa miaka 12 mfululizo, hawajawahi kupata tatizo la chakula.
Akizungumza mkoani hapa, Kanali Thomas amesema katika msimu wa mwaka 2021/2022 mkoa huo ulizalisha chakula tani 1,256,362, ambapo amesema mahitaji ya chakula mkoani humu kwa msimu wa mwaka 2022/2023 ni tani 469,172 na kuufanya mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 787,190.
Amesema chakula ambacho kilizalishwa katika msimu wa mwaka 2021/2022, kinatumika katika msimu huu wa mwaka 2022/2023.
“Mkoa wa Ruvuma ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara, kwa miaka minne mfululizo mkoa umeendelea na chakula la Taifa kwa kuongoza kitaifa katika uzalishaji wa chakula nchini,’’ alisema RC Thomas.
Akizungumzia mazao ya biashara, Kanali Thomas ameyataja mazao ya kimkakati yanayowaingizia, wakulima kipato kuwa ni zao la kahawa, ambapo katika msimu wa mwaka 2021/2022 jumla ya kilo milioni 13.7, ziliuzwa na kuingiza jumla ya shilingi bilioni 97.
Mazao mengine ya kimkakati ameyataja kuwa ni zao la ufuta, ambalo katika msimu uliopita limewaingizia wakulima shilingi bilioni 23.4, zao la soya limeingiza bilioni sita na zao la mbaazi limeingiza shilingi bilioni 1.3.
Amesema katika msimu ujao wa kilimo Mkoa wa Ruvuma, unahitaji mbolea tani 50,280, ambapo hivi sasa usajili wa wakulima kwa ajili ya mbolea ya ruzuku unaendelea na hadi sasa wakulima 216,366 wamejasiliwa kwenye vitabu.