RUWASA yataka wadau kutumia mpango wa WASH

DODOMA; Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imetoa mwito kwa wadau wa maji nchini kuutumia Mpango Kabambe wa WASH kila wilaya kama mfumo wa pamoja wa upangaji na uwekezaji, na si waraka unaomilikiwa na RUWASA pekee.
Akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa maji jijini hapa, Mwenyekiti wa Timu ya WASH Taifa (nawa, oga, osha) Singolile Mwamwaja alisema mpango kabambe huo unaweka upangaji wa pamoja, uwekezaji unaoratibiwa na uhamasishaji wa rasilimali.
“Mpango Kabambe wa Wash katika kila wilaya ((DWMP) unatoa msingi madhubuti zaidi wa kufikia huduma za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi zilizo endelevu, zenye usawa na zinazokidhi mahitaji ya wananchi,” alisema.
Mwamwaja alisema, DWMP ni mfumo wa pamoja, unaozingatia ushahidi na unaolenga uwekezaji, kwa ajili ya kupanga, kuratibu, kuweka vipaumbele, kutafuta na kuelekeza rasilimali.
Pia kufuatilia utekelezaji wa afua za maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi katika ngazi ya wilaya.
Pia RUWASA imeandaa mwongozo wa kufuata wakati wa utekelezaji wa Mpango Kabambe huo katika kila wilaya unaoweka utaratibu wa hatua kwa hatua.
Zinajumuisha maandalizi, tathmini katika ngazi ya wilaya, mipango ya muda mrefu na mipango ya muda mfupi.
Pia unahusisha uwekaji wa vipaumbele, uhamasishaji wa rasilimali na kuingiza afua zilizopewa kipaumbele katika michakato ya mipango na bajeti.
Amesema mwongozo unasisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau, uratibu, upangaji wa pamoja na uhamasishaji wa rasilimali, ili kuhakikisha kuwa mipango inamilikiwa na kutekelezwa kwa ufanisi na kuwa endelevu.
Wadau hao wameombwa kuthibitisha nia na dhamira yao ya kushiriki katika uandaaji wa Mpango Kabambe huo wa wilaya wa WASH.



