Ruzuku kutolewa mitungi ya gesi 452,445

DODOMA; SERIKALI imesema inafanya jitihada kuhakikisha bei ya nishati safi ya kupikia inapungua na kwa mwaka wa fedha 2024/25 itatoa ruzuku kwa mitungi 452,445 yenye thamani ya Sh Bilioni 10.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira aliyehoji kama serikali haioni haja ya kupunguza gharama ya gesi, ili lengo la kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2033/34 litimie.

“Serikali inafanya jitihada kuhakikisha bei ya nishati safi ya kupikia inapungua. Kwa upande wa mitungi ya gesi inayopatikana kutoka kwenye viwanda vya kusafisha mafuta (LPG – Liquified Petroleum Gas), ruzuku imetolewa kwa mitungi 83,500 yenye thamani ya Sh Bil 3.5.

“Aidha kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali itatoa ruzuku kwa mitungi 452,445 yenye thamani ya Sh Bil 10.

Kwa upande wa gesi asilia, Serikali inaendelea na uwekezaji wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha na kusambaza gesi majumbani.

“Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, ina mpango wa kuongeza miundombinu ili kupokea meli kubwa za gesi ya LPG na hivyo kushusha gharama za bidhaa hiyo.

“Pia, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi zinazojihusisha na usambazaji na uuzaji wa gesi ya LPG na gesi asilia pamoja na kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi vinavyohamishika na visivyohamishika kwa kila Wilaya,” amesema..

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button