Sababu 4 zatajwa kuimarika uchumi, Shilingi

DAR ES SALAAM; MWANASIASA mkongwe nchini, Stephen Wasira ametaja sababu nne zilizofanya uchumi kuimarika pamoja na kuongezeka thamani kwa Shilingi ya Tanzania.

Wasira alitaja sababu hizo kuwa ni utalii, madini, uuzaji wa zao la korosho nje ya nchi na kupunguza matumizi ya Dola za Marekani katika uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Alisema hayo juzi katika kipindi cha Mizani kilichorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).

Advertisement

Wasira alisema uchumi wa nchi ulishuka kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa dunia kutokana na janga la Covid-19, lakini kupitia utalii na madini uchumi sasa unaendelea kuimarika sambamba na kuongezeka kwa thamani ya Shilingi.

“Rais Samia (Suluhu Hassan) ametangaza utalii kwa kiwango kikubwa, hivi sasa watalii wanaoingia wamefikia milioni mbili, idadi ambayo ilikuwa haijafikiwa katika historia ya nchi yetu… eneo la pili ni madini sisi ni exporter (wasafirishaji) wa dhahabu nje ya nchi na dhahabu tumesafirisha imetuletea akiba ya dola… kwa hiyo madini yanatuletea Dola,” alisema Wasira.

Aidha, Wasira alilitaja zao la korosho kama sababu ya kuimarisha uchumi na kugusia kuongezeka kwa biashara ya kuuza bidhaa nje ya nchi kulinganisha na kununua kutoka nje.

“Maua mengine tunawapa wakulima wa korosho… zile zimetupa fedha ya kigeni imefanya value (thamani) ya Shilingi imepanda dhidi ya Dola na si kwamba Dola imeshuka, hapana Dola ipo vilevile duniani,” alisema.

Aliongeza: “Uchumi mzuri ni kuwa lazima uuze zaidi… kwa hiyo tunapouza zaidi na kununua vilivyo vya lazima ili kutotumia thamani ya Shilingi… kwa hiyo Shilingi inapokuwa na nguvu mtu ukiagiza kutoka nje inafanya mtu wa hapa anapata nafuu ya maisha”.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Marcellina Chijoriga amefafanua zaidi sababu za uchumi kuimarika.

“Katika suala la Dola tumepunguza uagizaji wa vitu, tumeagiza vitu ambavyo vinaleta thamani kwenye uzajilishaji wetu… Shilingi inapoongezeka thamani kwa nchi inapata faida,” alisema.

Aliongeza: “Ile nakisi (kuuza na kununua bidhaa nje ya nchi) ndio jibu kubwa lazima tukitaka uchumi mzuri ni lazima nakisi yetu tupunguze sana kwa maana ni lazima tuuze zaidi vitu nje… Serikali inajitahidi kupunguza uagizaji wa vitu nje.

“Pia viongozi hawa wametoa ushauri na kuhimiza uwekezaji wa wazawa. Ili kupunguza athari ya uagizaji vitu vingi kutoka nje lazima uzalishaji wa ndani uongezeka turudi kwenye pamba (akitolea mfano uzalishaji wa zao la pamba) zamani kulikuwa na viwanda vya Mwatex kulikuwa na Urafiki walau hizi pambapamba, kanga na batiki zilikuwa zinatengenezwa hapa Tanzania sasa hii ilikuwa inapunguza sana ile kutegemea vitu kutoka nje,” alisema.