SADC, EAC zatakiwa kuendeleza matumizi bora ya nishati

WAZIRI  wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki( EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika  (SADC) kuendeleza teknolijia ya matumizi bora ya nishati

Amesema maendeleo ya viwanda yanategemea uwepo wa nishati ya kutosha haswa katika kuinua uchumi

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa kufunga mkutano wa kikanda wa matumizi bora ya nishati uliohusisha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika leo jijini Arusha.

Advertisement

Amesema lengo la nchi ni kuendelea kukuza uchumi, viwanda vifanye kazi na biashara zifanyike kwa ufanisi lakini hilo litawezekana ikiwa kuna nishati ya kutosha ambayo uwepo wake unategemea usahihi katika matumizi yake.

Amesema Tanzania ina matumizi bora ya nishati ambapo kwa sasa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango fanisi vya vifaa vya nishati vinavyozalishwa au kuingizwa nchi ambavyo vitawezesha nchi kutumia umeme kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk Khatibu Kazungu amesema serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati imejipanga kutekeleza mkakati wa matumizi bora ya nishati uliozinduliwa Desemba 4, 2024  kwa kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kwa kuwekewa bajeti ili nchi iweze kuwa na fanisi katika vifaa vya nishati.

Amesema kupitia Mkutano wa REEC 2024 maazimio mbalimbali yamefikiwa ikiwemo kufanya tafiti za pamoja ili kuboresha matumizi bora ya nishati na kuihusisha kikamilifu sekta binafsi.