SADC yataka uratibu imara uwekezaji madini Afrika

DAR ES SALAAM: Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imetoa wito wa kuimarishwa kwa uratibu kati ya serikali na sekta binafsi ili kuharakisha uwekezaji katika sekta ya madini na kukuza viwanda, wakati mataifa ya Afrika yakisaka udhibiti mkubwa wa rasilimali muhimu zinazozidi kuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko ya nishati duniani.
Wito huo ulitolewa katika Jukwaa la Kiwango cha Juu la Mawaziri wa SADC kuhusu Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi katika Madini, lililofanyika sambamba na mkutano wa uwekezaji wa madini barani Afrika wa mwaka 2026 mjini Cape Town.
Viongozi wa ukanda huo walionya kuwa Afrika ipo hatarini kubaki msambazaji wa malighafi iwapo haitachukua hatua madhubuti kuelekea kuongeza thamani ya madini na kuwa na sera shirikishi za viwanda.
Msukumo huo mpya unakuja wakati mahitaji ya kimataifa ya madini muhimu kama lithiamu, kobalti, grafaiti, nikeli na madini adimu (rare earth elements) yakiongezeka, yakitumika katika magari ya umeme, betri na miundombinu ya nishati jadidifu.
Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Mpedi Magosi, alisema ni lazima ukanda huo uhakikishe uchimbaji wa madini unachangia ukuaji wa viwanda kwa muda mrefu badala ya kuendelea kutegemea mauzo ya malighafi.
“Changamoto yetu haijawahi kuwa uhaba wa rasilimali, bali ni kuongeza thamani,” alisema Magosi katika mkutano wa Baraza la SADC uliofanyika Machi mwaka huu.
Serikali za Afrika sasa zinatafuta upya nafasi ya bara hilo katika minyororo ya thamani ya madini duniani, zikisisitiza kuwa miongo ya kuuza malighafi bila kuchakatwa imechangia kwa kiwango kidogo maendeleo ya viwanda licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali.
Hoja hiyo imepata uzito zaidi wakati mataifa makubwa kama China, Marekani na Umoja wa Ulaya yakiongeza ushindani wa kupata madini muhimu kwa ajili ya viwanda vya kisasa na teknolojia za nishati safi.
Katika jukwaa hilo la Cape Town, mawaziri na wadau wa sekta ya madini walisisitiza umuhimu wa sera za pamoja za kikanda, uwekezaji katika miundombinu na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuongeza ushindani na kuvutia mitaji ya muda mrefu katika uchimbaji na uchakataji wa madini.
Maofisa wa kikanda pia walisisitiza haja ya Afrika kujadiliana kwa pamoja masuala ya madini ili kuongeza nguvu ya majadiliano katika ngazi ya kimataifa.
Mjadala huo unaakisi mabadiliko mapana barani humo, ambapo serikali zinaanza kuanzisha sera za kuongeza thamani ya ndani, kuweka vikwazo vya usafirishaji wa malighafi na kuongeza ushiriki wa serikali katika sekta ya madini ili kunufaika zaidi na rasilimali hizo.
Nchi kama Zimbabwe, Namibia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeanza kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa madini muhimu au kuhamasisha uchakataji wa ndani kama sehemu ya mikakati ya kukuza viwanda.
Wachambuzi wanasema hatua hizi zinalenga kuepuka historia ya kampuni za kigeni kuchimba madini na kuondoka bila kuacha manufaa makubwa kwa uchumi wa ndani.
Hata hivyo, wawekezaji wanaonya kuwa kutokuwepo kwa uhakika wa sera, upungufu wa miundombinu na changamoto za upatikanaji wa fedha vinaweza kudhoofisha jitihada za kuvutia uwekezaji.
Viongozi wa SADC walikiri changamoto hizo na kusisitiza umuhimu wa kuwa na sera zinazoeleweka na mifumo ya kikanda iliyoratibiwa ili kuongeza imani kwa wawekezaji.
Aidha, walieleza kuwa ushirikiano kati ya serikali, kampuni za madini na jamii ni muhimu ili kuhakikisha ukuaji wa uwekezaji unaendana na ulinzi wa mazingira, ajira na utulivu wa kijamii.
Msukumo huo wa kuongeza udhibiti wa rasilimali za madini unaendana na Mkakati wa Viwanda wa SADC pamoja na jitihada pana za bara la Afrika kupitia Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA) zinazolenga kujenga minyororo ya thamani ya viwanda inayohusisha sekta ya madini na nishati.



