JESHI la Polisi mkoa wa Morogoro linamshikilia mwanamke Salipina Thomas (21) mkazi wa kitongoji cha Temekero, kijiji cha Kiroka, Wilayani Morogoro kwa tuhuma za mauaji ya Rashid Said Mahalangande (20) ambapo wawili hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa, Fortunatus Musilimu amesema Septemba 17, 2022 kuwa mauaji hayo yalitokea majira ya saa nane usiku wa kuamkia Septemba 16, mwaka huu kitongoji cha Temekero.
Musilimu amesema mauaji hayo yanahusishwa na wivu wa kimapenzi ambapo kijana aitwaye Richard Stephen Chanzila (23) mkazi wa Kitongoji cha Maembe, Kijiji cha Kiloka ndiye anatuhumiwa kutekeleza mauaji hayo.
Kamanda Musilimu amesema, mtuhumiwa huyo inadaiwa alimkata na kitu chenye ncha kali shingoni kijana Mahalagande (20), mkazi wa Sultan Area, Manispaa ya Morogoro ambaye pia alikuwa akijishughulisha na bodaboda.
Musilimu amesema kuwa, chanzo ni wivu wa mapenzi ambapo marehemu alikutwa amelala ndani ya nyumba Salipina ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa kitongoji Temekero ambaye ni mzazi mwenzake na pia walikuwa na mahusiano.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa kuwa, baada ya kuwakuta wamelala kwenye nyumba ya huyo mzazi mwezake ndipo alipomkata Mahalagande sehemu ya shingoni kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Amesema baada ya Mahalagande kukatwa na kitu chenye ncha kali, mwanamke huyo alifanikiwa kukimbia na kwenda kuomba msaada.
Musilimu amesema, Chanzila baada ya kufanya mauaji hayo aliubeba mwili wa marehemu na kwenda kuutupa porini umbali wa mita 100 kutoka eneo alilofanyika mauaji.
Amesema mtuhumiwa huyo alikimbia kijijini hapo kwenda kusikojulikana baada ya mauaji hayo na Polisi inaendelea kumtafuta ili kumtia mbaroni na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili kuchukua mkondo wake.
“Nawasihi wananchi ya kwamba kufanya mauaji ya aina mbalimbali kutokana na mapenzi, ushirikina au migogoro mbalimbali sio maamuzi sahihi , ni kinyume cha sheria , zipo njia ambazo zinaweza kutumika kupata suluhu ya mambo yanayojitokeza badala ya kuchukua maamuzi ya kuua mtu” amesema Musilimu.
Musilimu ameishauri jamii ya kwamba badala ya kuchukua maamuzi ya kuua mtu , ni vyema watumie njia mbalimbali kutusaidia kupata suluhu ya changamoto wanazokabiliana nazo kimaisha .