SALUM SUED ‘KUSI’ aitabiria ubingwa Taifa Stars CHAN

SALUM Sued maarufu kama ‘Kusi’ ni mmoja wa mabeki bora wa kati Tanzania ilibahatika kuwa nao hasa baada ya kizazi cha kina Deo Njohole ‘OCD’, George Masatu, Frank Kassanga ‘Bwalya’, Godwin Aswile na wengineo.

Kusi anatokea ukoo wa mpira wa miguu kwa maana ya baba yake Hamis Sued aliyekuwa mchezaji mahiri kwenye klabu ya Pan African miaka ya 1980 lakini pia mdogo wake Said Sued ‘Panuci’ amewahi kutamba kwenye timu ya Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Beki huyo mwenye mwili uliojengeka hasa kimpira, nyota yake ilianza kung’ara baada ya kusajiliwa na mabingwa mara 31 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga mwishoni mwa mwaka 1999 na kuanza kuitumikia kwenye mashindano mwaka 2000.

Kusi alijiunga na Yanga akitokea klabu ya vijana ya Ilala aliyokuwa akicheza pamoja na mdogo wake Said Sued aliyemudu nafasi ya beki wa kulia.

Wakati anajiunga na Yanga, Kusi aliwakuta wachezaji wengi wenye majina makubwa na wazoefu wakati ule kama marehemu Said Mwamba ‘Kizota’ Sekilojo Chambua, Edibily Lunyamila, Salvatory Edward, Mtwa Kihwelo, Eustace Bajwala, Bakari Malima na wengineo.

Akiwa bado kijana mdogo na chipukizi kwenye klabu hiyo yenye mashabiki wengi wa soka Tanzania, Kussy hakusita kummwagia sifa mchezaji mkongwe na mwenye kipaji kikubwa zaidi wakati huo, Said Mwamba ‘Kizota’. Anasema akiwa na Yanga kuna kipindi alitaka kukata tamaa na kufikiria kuachana na soka kabisa lakini Kizota alimsaidia kwa kumpa ujasiri.

“Kizota ni mmoja kati ya watu walionisaidia sana pale kuwa na ujasiri, alinichukulia kama mdogo aitabiria ubingwa Taifa Stars CHAN wake na nafikiri damu zetu ziliendana na nilikuwa napatana naye sana,” alisema Kusi. Akimuelezea Kizota, Kussy anasema alikuwa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani.

“Kwa ufupi alikuwa ni mchezaji anayejua sana soka, ukimpa namba yoyote anacheza kwa jinsi ya hiyo namba inavyotaka na wengi walikuwa wanamuona kama mchezaji mkorofi lakini hakuwa hivyo, Kizota ni mpaka wewe umkorofishe ndipo utakapomuona mkorofi,” alisema Kusi.

“Nje ya uwanja ni mtu mmoja poa sana kwa sababu hakuwa na mambo mengi, yeye ni mtu mkimya sana sio mwongeaji sana, yeye na mitungi yake, hana habari na mtu,” anaongeza. Anasema ukorofi wake ni mpaka wewe umchokoze, vinginevyo hakuwa na habari na mtu wala hakuwa mtu wa kujichanganya sana.

“Ukorofi wake ni mpaka wewe umzingue, vinginevyo hana habari na mtu na hakuwa mtu wa kujichanganya sana, yeye alikuwa na watu wake ambao anaweza kukaa nao,” anasema Kusi kuhusu Kizota. Kuhusu jina la Kusi anasema aliitwa hivyo tangu akiwa mtoto na alijikuta akiitwa hivyo na marafiki zake wengi bado wanamuita kwa hilo jina.

“Jina hili nilijikuta nimepewa tu hata sijui lilitokana na nini, nimeona watu wananiita tu Kusi toka utotoni kiasi kwamba hata jina langu la Salum nikawa silitumii sana na marafiki zangu wengi wananijua kwa jina la Kusi,” anasema. Kusi anazungumzia uamuzi wake wa kuondoka Yanga na kujiunga na Moro United kuwa ilikuwa kwa ajili ya maisha yake.

“Ilibidi kwa ajili ya maisha yangu niondoke tu, miaka yote niliyokaa Yanga hakuna kitu nimepata cha maana zaidi ya kudhulumiwa na kupewa pesa kwa mafungu ambazo haziwezi kufanya kitu cha maana,” anasema Kusi.

Kussy anakumbuka mara yake ya kwanza kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ilikuwa mwaka 2004 na kocha Msindo Msolla kwenye mchezo wa kutafuta kucheza fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Zambia ingawa hakucheza mchezo huo.

“Kipindi kile wengi waliokuwa wanaanza hasa kwenye nafasi yangu ni wachezaji waliokuwa Simba maana ndiyo timu iliyokuwa inafanya vizuri na hauwezi kupinga hilo, kwanza walikuwa wanacheza mashindano ya kimataifa na walikuwa wanajitahidi, kwa hiyo lazima aanze na wale,” anasema Kusi.

Mabeki wa kati wa Simba kipindi hicho walikuwa Victor Costa, Amri Said na Boniface Pawasa. Kusi anayakumbuka michuano ya Mabingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2009) nchini Ivory Coast anasema yalikuwa mazuri na yalifuatiliwa sana na mashabiki.

“Yalikuwa makubwa nadhani hata ufuatiliaji wake ulikuwa mkubwa pia kwa sababu ndiyo yalikuwa yanaanza kufanyika kama sijakosea, kila mmoja alikuwa na hamu ya kutaka kuona hayo mashindano yatakuwaje, tofauti na sasa hivi,” anasema Kusi. Kusi anasema kwenye fainali hizo walikosa bahati baada ya kutolewa na Zambia waliokuwa wanahitaji sare kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za mwisho.

“Nafikiri tulikosa tu bahati, maana mechi yetu ya kusonga mbele ilikuwa dhidi ya Zambia, wao wanahitaji sare na sisi ushindi. Tulikuwa tunaongoza mpaka dakika ya mwisho, wakasawazisha baada ya sisi kukosa penalti maana kama tungepata ile penalti, tungesonga mbele,” alisema Kusi.

Baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars kwenye fainali zile za Ivory Coast ni marehemu Godfrey Bonny, Nurdin Bakari, Jerry Tegete, Nizar Khalfan, Abdi Kassim, Shadrack Nsajigwa, Danny Mrwanda, Mrisho Ngassa na wengineo.

Akijibu swali kama kuna tofauti ya kikosi cha sasa cha Taifa Stars na cha wakati wao, Kusi anasema soka limebadilika hivyo lazima kuwe na tofauti.

“Utofauti lazima uwepo maana mwaka 2009 hadi sasa imepita miaka mingi hapo kwa hiyo lazima kuwepo na tofauti ya kiuchezaji na kimbinu kwa sababu soka linabadilika kila wakati, vitu vipya vinaingia, ndiyo maana unaona mifumo ya uchezaji toka enzi na enzi ni ileile lakini inachezwa tofauti na ilivyoanza,” alisema Kussy.

Hata hivyo Kusi anasema anaipa nafasi kubwa Taifa Stars kushinda ubingwa wa CHAN kwa sababu kwa vikosi vya wachezaji wa ndani wako vizuri na asilimia kubwa ya wachezaji ni walewale hata wanaposhiriki mashindano mengi yanayohusisha wachezaji kutoka nje ya ligi za Afrika.

Kusi aliyepewa heshima ya kuigwa kutokana na utumishi wake mzuri na wa muda mrefu kwenye kikosi cha Taifa Stars anasema hakupewa zawadi yoyote zaidi ya kuagwa kwenye mchezo dhidi ya Uganda, Uwanja wa CCM Kirumba, kitu alichosema ni kikubwa zaidi kwake.

“Ile mechi tulicheza na Uganda na hakuna zawadi yoyote niliyopewa zaidi ya kuagwa kwa kucheza ile mechi na nadhani ndilo kubwa na la heshima kuliko lolote,” anasema Kusi.

Beki huyo aliyeitumikia Mtibwa Sugar kwa kipindi kirefu anasema pamoja na kucheza na kushuhudia wachezaji wengi kabla na baada yake, alivutiwa na wachezaji mbalimbali kama vile Ulimboka Mwakingwe na mdogo wake Said Sued ‘Panuci’ wa Simba na Waziri Mahadhi ‘Mendieta’ aliyecheza naye Yanga.

Kwa waliomtangulia alikuwa akivutiwa na mabeki Frank Kasanga ‘Bwalya’ na Godwin Aswile huku kwa
wachezaji wa sasa anakoshwa na Ibrahim Hamadi ‘Bacca’, Dickson Job wa Yanga na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa
Azam.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button