RAIS Samia Suluhu Hassana amebainisha mambo matatu waliyozungumza katika Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali zenye Uchumi Mkubwa zaidi Duniani (G20) uliofanyika Brazil, mojawapo ikiwa ni ajenda ya nishati safi ya kupikia na mikakati ya kupunguza njaa.
Rais Samia alibainisha hayo wakati wa mahojiano baina yake na wahariri wa vyombo vya habari nchini baada ya kukamilika kwa mkutano huo Novemba 19, mwaka huu.
Alisema walizungumza kuhusu mikakati ya kupunguza njaa na kuwa walifanya tathmini ni kwa kiasi gani dunia inaweza kuondoa tatizo hilo.
Alieleza kuwa ilionekana kuwa kazi haijafanyika vizuri kwa sababu wapo watu wengi duniani wana tatizo la njaa na si Afrika pekee bali pia nje ya bara.
“Kwa upande wetu tulipopewa nafasi ya kusema kwenye hili tulizungumza hali halisi kwamba tukienda hali hii ilivyo bila kupigwa na matukio yoyote ya mabadiliko ya tabianchi, basi tunajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128 na tunaweza tukawauzia wenzetu,” alieleza.
Alisema Tanzania ina uwezo wa kuzalisha zaidi na kulisha nchi za jirani na Afrika na nje ya bara. Kwa sasa inasafirisha mazao ya mbogamboga kwenda nchi za Ulaya na inasafirisha nchi jirani mahindi, mpunga na kuilisha China maharage ya soya.
Pamoja na hayo, alisema vipo vikwazo kama vile ukosefu wa mashine za kisasa, mbolea ya kutosha na tafiti kwenye kilimo na vikitafutiwa ufumbuzi itakuwa rahisi kutimiza lengo la kuilisha Afrika na dunia kwa ujumla.
Aidha, alisema mkutano huo pia ulijadili kuhusu nishati jadidifu na kueleza kuwa Tanzania ipo kwenye safari ya kutoka kwenye matumizi ya dizeli kwenda kwenye nishati jadidifu inayotokana na maji na upepo.
“Sisi wengine bado tupo kwenye safari, bado tunatumia dizeli kwa mfano bwawa letu la Julius Nyerere tunatumia nishati ya maji ambayo ndio nishati jadidifu lakini kwa sasa tuseme asilimia 60 ya umeme wetu inatokana na gesi,” alisema.
Aliongeza, “Wanapigia kelele tusitumie gesi lakini ni safari na sisi tumesema kwa nchi za Afrika tumeomba huko tunapokutana tutumie gesi mpaka inapofika mwaka 2050.”
Soma pia:Rais Samia kufanya ziara ya kikazi Brazil
Aidha, Rais Samia alisema alizungumzia ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo amekuwa kinara wa kuipigia chapuo na kuwataka washiriki wa mkutano huo waiunge mkono kuhakikisha watu wengi Afrika wanapata umeme kutoka katika vyanzo vya maji, jua na upepo.
“Jambo la tatu tulizungumza mambo ya utawala bora na utawala wa sheria, hapo sasa sisi wengine tulikuwa wasikilizaji lakini yaliyosemwa mule ni haja ya kuona ulimwengu unakuwa salama, haja ya kusimamisha vita vinavyoendelea, haja ya kutoa njia kusaidia wale waliofikwa na maafa ya vita na maafa mengine,” alieleza Rais Samia.
Wakati huo huo alisema alikutana na viongozi wa nchi mbalimbali katika mikutano ya pembeni na kujadili maeneo tofauti ya ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania.
Miongoni mwa maeneo ni mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere unaotekelezwa kwa ushirikiano na Misri, miradi ya mafuta na gesi ambayo Tanzania inashirikiana na Indonesia na ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo alijadiliana na Waziri Mkuu wa Norway