RAIS Samia Suluhu Hassan ameanika namna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanavyoghushi risiti za mashine za EFDs na stempu za kodi kwa vinywaji na kuiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukomesha mara moja wizi huo aliouita dhuluma kwa Watanzania.
Rais Samia amezungumzia suala hili wakati akitoa hotuba kwenye tukio la utoaji wa tuzo za walipakodi bora kwa mwaka 2023/2024 lililofanyika Dar es Salaam.
Aliitaka TRA kuwa macho na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, wanaoghushi risiti na stempu hizo kuiibia serikali.
“Ninazo taarifa kuhusu vitendo vya kughushi stempu kwenye bidhaa za vinywaji ili kuiba kodi za ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji hivyo. Najua kuna sakata limetokea hivi karibuni na TRA isingeamka mapema tulikuwa tunapata hasara ya bilioni 200 zinazokwenda kupotea kwenye mikono isiyo halali,” alieleza.
Alisema pia, anafahamu kuhusu ujanja wa baadhi ya kampuni zinazokwepa kodi kwa njia ya kutotoa risiti na kughushi risiti za EFDs.
“Nawataka TRA msimame kidete na kuchukua htua kali dhidi ya uhalifu huu. Tunapotoa tuzo kama hizi ni vizuri pia, tukatoa adhabu kwa wale wote wanaotulazimisha kutumia nguvu kudai kodi,” alisisitiza.
Alimtaka Kamishna Mkuu wa TRA kusimamia haki na usawa kwa walipakodi.
Akizungumzia suala la ufanisi wa TRA, Rais Samia alisisitiza ni muhimu kwa watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi kwa uadilifu ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kuleta mafanikio zaidi.
Alisema lazima hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya watumishi wanaohusika na vitendo vya rushwa na ukwepaji
kodi.
“Mazingira hayo ndiyo yanayochochea rushwa, ambayo sio tu ni adui wa haki, bali pia ni adui kwa maendeleo yetu,” aliongeza.
Alisisitiza serikali inatambua mchango wa walipakodi na kuwaomba wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa uaminifu ili kusaidia kufikia malengo ya kitaifa.
Alisema serikali inaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kuwezesha
wafanyabiashara na walipakodi kutimiza wajibu wao kwa urahisi.
Rais Samia pia, alizungumzia mpango wa serikali wa kupunguza utegemezi wa kibajeti kwa kukuza mapato ya ndani, akisema lengo ni kujenga mfumo wa kodi unaotabirika, wenye usawa na usio na usumbufu kwa walipakodi.
“Tunataka kuwa na mfumo wa kodi utakaorahisisha na kuchagiza kukua kwa shughuli za kiuchumi ili kodi ikusanywe kwa wingi na kujiimarisha kimapato na kujenga taifa lenye kujiamini,” alisisitiza.
Katika kutekeleza dhamira hiyo, Rais Samia alisema kuwa mwaka jana, serikali iliunda Tume ya Maboresho ya Kodi
ili kufanya tathmini ya mifumo ya sasa ya kodi na kuleta mapendekezo ya kuboresha na kuimarisha mifumo hiyo.
Alieleza kuwa mwelekeo wa serikali ni kuimarisha mazingira ya biashara na kutoa huduma bora kwa walipakodi ili kukuza ajira na kuongeza mapato ya serikali.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alitangaza kuwa kuanzia mwaka ujao, tuzo za walipakodi bora zitakuwa chini ya Rais, badala ya TRA, lengo likiwa ni kutoa hadhi zaidi kwa siku hii na kuwapa motisha wafanyabiashara wanaoonesha uzalendo kwa kulipa kodi.
Pia, alielezea umuhimu wa kuongeza idadi ya walipakodi, akisema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inataka serikali kupunguza utegemezi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Aliomba wafanyabiashara, hasa wa sekta isiyo rasmi, kuhamasika na kuingia kwenye sekta rasmi kusaidia kuongeza
mapato ya taifa.
“Ni lazima tuweke sera na mikakati itakayofanya sekta isiyo rasmi ihitimu na kuingia kwenye sekta rasmi,” alisisitiza.
Rais Samia alisisitiza serikali itaendelea kutoa mazingira bora ya kufanya biashara kwa kuwasaidia wafanyabiashara, huku ikiwahamasisha kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi.
Aliwataka wafanyabiashara kuwa mabalozi wema kwa jamii zao, wakisisitiza kuwa ulipaji wa kodi ni uzalendo na ni hatua muhimu kwa ustawi wa taifa.
Katika tukio hilo TRA ilitangaza Benki ya NMB, Tanzania Breweries Company na CRDB Bank, kuwa washindi bora wa kulipa kodi kwa hiari huku Kampuni ya Bakhressa ikitangazwa kwa upande wa sekta binafsi.