Samia acharuka ukwepaji kodi

Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kodi ya serikali lazima ilipwe na asitokee mtu yeyote anayetaka kukwepa kulipa kodi kwa kisingizio cha kupata maelekezo kutoka kwake.

Rais Samia amesema hayo Dar es Salaam kwenye hafla ya Utoaji Tuzo kwa Walipa Kodi Bora kwa Mwaka 2023/2024 na kuwataka viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wasidanganywe na yeyote.

Amesema kama ikitokea kukawa na mlipa kodi atakayepata hiyo nafasi ya kutolipa kodi kutoka kwake, atatoa maelekezo kwa njia ya maandishi na si mtu atoe maelekezo yake binafsi akidai ni maelekezo kutoka juu.

Advertisement

“Kodi ya serikali lazima ilipwe, msidanganywe na yeyote. Mimi sijawahi kutoa maelekezo ya mtu asilipe kodi na ikitokea nitatoa maelekezo kwa maandishi na sio mtu awaambie haya ni maelekezo kutoka juu,”amsema Rais Samia.

Amesema ubunifu wa tuzo za walipa kodi ni mzuri ukiwa na lengo la kutoa motisha kwa walipa kodi kwa sababu kodi inayokusanywa inatumika kwa maendeleo ya taifa.

Rais Samia ameitaka TRA kutoa adhabu kwa walipaji wa kodi wanaosubiri hadi kuwe na matumizi ya nguvu ndio walipe kwani ulipaji wa kodi ni lazima kwa maendeleo ya nchi.

Aidha, Rais Samia amesema ili kuipa thamani zaidi programu ya utoaji wa tuzo kwa walipakodi, kuanzia mwakani, shughuli ya utoaji wa tuzo kwa walipakodi haitafanywa na TRA bali itafanywa na yeye na itaitwa Tuzo ya Rais ya walipa kodi.

Mbali na hayo, Rais Samia hakuacha kuikemea TRA kwa kuchukua kodi isiyostahili kutoka kwa walipa kodi akisisitiza kuwa lazima kodi ilipwe kwa haki na kusiwe na uonevu kwa wananchi.

Amewataka TRA pia kuwa macho na walipa kodi ambao wanaghushi risiti na kuisababishia hasara serikali kwa
sababu huoni ukwepaji kodi na wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

Rais Samia aliwaagiza watumishi wa TRA kuhakikisha kuwa wanafanyakazi kwa uadilifu na kuwaonya dhidi ya vitendo vya rushwa huku akiutaka uongozi kuwawajibisha wote watakaohusika.