Samia ahimiza utu na weledi

Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi kwa salamu za kheri na upendo katika kumbukizi ya miaka minne tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania.

Aliapishwa Machi 19, 2021 katika Ikulu ya Dar es Salaam kuwa, Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita baada ya kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

“Tuungane pamoja kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu, tudumu katika umoja, amani na utulivu,” aliandika Rais Samia katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamiii wa X.

Advertisement

Aliongeza: “Tumuombe pia Mwenyezi Mungu aendelee kutuongoza katika utu na weledi kwenye utekelezaji wa majukumu yetu, na kuzibariki kazi tunazozifanya katika kuleta ustawi wa nchi yetu na Wananchi wote. Kazi na Utu, Tunasonga Mbele”.

Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema, Rais Samia ametekeleza ahadi yake kwa Watanzania.

Majaliwa amesema, Rais Samia alipotoa hotuba ya kwanza bungeni Dodoma aliahidi miradi yote itaendelezwa na mingine mipya itaanzishwa.

Alisema hayo katika kongamano la kumpongeza, Rais Samia kwa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake lililoandaliwa na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza, juzi.

Majaliwa alisema, Rais Samia amesimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ya huduma za jamii inayowagusa wananchi hadi vijijini kwenye sekta za afya, elimu na maji.

Alisema mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida, Dodoma na Mara itanufaika na miradi ya maji ya Ziwa Victoria.

Kuhusu afya alisema serikali imewekeza katika miundombinu ya kutolea huduma za afya, dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi ya kata hadi taifa.

Katika nishati ya umeme alisema wilaya na vijiji vyote vimepatiwa umeme na hivi sasa serikali inasambaza nishati kwenye vitongoji na visiwa.

Akizungumzia kilimo, alisema serikali imeimarisha mifumo ya masoko ya zao la pamba kwa kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umepandisha bei ya zao hilo.

Mratibu wa kongamano hilo, Aloyce Nyanda alisema kazi zinazofanywa na serikali zina manufaa kwa wananchi ndiyo maana yeye na waandishi wenzake wa habari waliamua kujadili mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema, Rais Samia amegusa maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk Doto Bulendu alisema wakati, Rais Samia anaingia madarakani kulikuwa na mashaka kama angeweza lakini amethibitisha anaweza.

 

 

 

Imeandikwa na Waandishi Wetu, Dar na Nashon Kennedy, Mwanza

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *