RAIS Samia Suluhu Hassan ameteua viongozi na amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.
Katika mabadiliko hayo Rais Samia amehamisha majukumu ya sekta ya habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuunda wizara mpya ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Taarifa iliyotolewa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka imeeleza kuwa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Profesa Kabudi alikuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kabla ya kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli kuwa mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Aidha, Rais Samia amemteua Jerry Silaa kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kabla ya uteuzi huo Silaa alikuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Dk Damas Ndumbaro ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akitoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mbali na wizara hizo, Dk Ndumbaro aliwahi pia kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na baadaye alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria kabla ya kuhamishwa na sasa kurudishwa tena.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akichukua nafasi ya Dk Ashatu Kijaji.
Dk Kijaji ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi akichukua nafasi ya Abdalla Ulega. Awali, Dk Kijaji alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ulega ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi akichukua nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Rais Samia amemteua Gerson Msigwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Awali, Msigwa alikuwa mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kisha akawa Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, Ikulu, na baadae akachaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.
Dk James Kilabuko ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).
Kabla ya uteuzi huo Dk Kilabuko alikuwa Katibu Msaidizi wa Baraza la Mawaziri (Maendeleo ya Jamii).
Dk Stephen Nindi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji.
Rais Samia amemhamisha Dk Suleiman Serera kutoka Wizara ya Kilimo kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara na Balozi Dk John Simbachawene atapangiwa kituo cha kazi.
Amemteua pia Profesa Mohamed Janabi kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Afya na Tiba, na pamoja na nafasi hiyo Profesa Janabi ataendelea kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Amemteua pia Anderson Mutatembwa kuwa balozi na atapangiwa kituo cha kazi.
Msemaji Mkuu wa Serikali wa zamani, Mobhare Matinyi ameteuliwa kuwa Balozi na atapangiwa kituo cha kazi.
Rais Samia amemteua Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad kuwa balozi na atapangiwa kituo cha kazi.
Kamishna wa Polisi, Suzan Kaganda ameteuliwa kuwa balozi na atapangiwa kituo cha kazi.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba ameteuliwa kuwa balozi na atapangiwa kituo cha kazi.
Katika hatua nyingine, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limewapongeza Waziri Profesa Palamagamba Kabudi na Msigwa.
“Faraja tuliyoipata ni kwamba viongozi wakuu wote walioteuliwa kuongoza wizara hii mpya ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri na Katibu Mkuu wote ni waandishi wa habari kitaaluma. Tunaamini hawataipa kisogo sekta ya habari,” alieleza Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.