Samia asisitiza haki uchaguzi wa serikali za mitaa

DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa haki, demokrasia, sheria na utawala bora utadumishwa kwa watu wote wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Rais Samia ameyasema hayo katika sherehe za mwaka mpya 2024 kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa zilizofanyika Ikulu.

Aidha Rais Samia amesema ili kuhakikisha uchaguzi huru na haki kikosi kazi huru cha kupitia na kushauri mageuzi muhimu katika mfumo wa siasa kiliundwa ambapo kiliwasilisha ripoti yake mwaka 2023.

Advertisement

Amesema mapendekezo mengi ya kikosi kazi yalipokelewa na serikali na wadau wote yalihusu kuongeza uwazi katika michakato ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.

Rais Samia amesema masuala machache hayakupokelewa moja kwa moja ambayo yalikuwa ni kinyume na katiba hivyo yanaweza kuchuuliwa wakati wa mchakato wa marekebisho ya katiba.