RAIS Samia Suluhu Hassan ametaja changamoto tatu katika majengo kwenye eneo la Kariakoo mkoani Dae es Salaam.
Ametaja changamoto hizo Ikulu Dar es Salam wakati wa hafla ya chakula cha mchana na walioshiriki kazi ya uokozi baada ya jengo la ghorofa kuanguka Kariakoo Novemba 16, mwaka jana.
Amesema ajali ya kuporomoka kwa jengo la Kariakoo imetoa somo jinsi biashara inavyoendeshwa ndani ya majengo mengi katika soko hilo.
Rais Samia alitaja changamoto hizo ni pamoja na majengo mengi kuzidiwa na uzito wa mizigo.
“Tumeelezwa jengo lilikuwa na uwezo wa kuchukua tani 250 za mizigo lakini tani zilizokuwa pale ni 850, kwa hiyo kwa vyovyote lisingeweza kubeba na hilo ni jengo moja. Nina hakika majengo mengi yaliyopo Kariakoo yapo katika mfumo huo,” alisema.
Aliongeza, “utanuzi wa majengo unafanywa kwa msingi uleule uliopo mwanzo na si kuanza upya, tunarefusha juu, tunachimba chini lakini kwa msingi uleule , hii ni hatari.”
Rais Samia alitaja changamoto nyingine kuwa ni usimamizi hafifu wa serikali wakati wa ujenzi katika kuhakikisha viwango vya ujenzi vinazingatiwa. “Usimamizi wa serikali wakati wa ujenzi na kuhakikisha viwango vya ujenzi unafuatwa, kwa walioliona jengo tulikuwa tunaona mchanga mwingi kuliko saruji,” alisema.
Rais Samia alisema ajali ya Kariakoo imeonesha mambo mengi, likiwemo suala la uwepo wa mali ambazo hazilipiwi kodi.
“Mimi nililiona kwa haraka haraka na pengine huleta mzozo ni mali inayofichwa mle ndani na pengine bila kulipiwa kodi. Sidhani kama zile tani 850 zimelipiwa kodi na ndio ulikuwa ugomvi mkubwa kwa TRA wanapopeleka watu kukagua maghala ndani ya Karikaoo,” alisema.
Rais Samia alisema kupitia ajali ya Kariakoo, serikali inakuja na mipango ya kuzingatia ili kukabiliana na majanga yanapotokea. Alisema serikali itahakikisha kunakuwa na vifaa, wataalamu na rasilimali ili kukabiliana na maafa kwa
ufanisi.
Pia, alisema serikali itaimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa, ikiwemo mifumo ya tahadhari pamoja na kuwajengea uwezo kamati ya usimamizi wa maafa katika ngazi za mikoa na wilaya.
Rais Samia alisema kuanzia sasa serikali itahakikisha viwango vya ubora katika ujenzi wa majengo vinazingatiwa.
“Tutahakikisha viwango vya ubora na ujenzi vinazingatiwa ipasavyo na taratibu za ukaguzi wa majengo zinaimarishwa, sheria za ujenzi zinafuatwa na rasilimali za kiufundi zinapatikana,” alisema.
Alimuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo asimamie ushindani katika biashara kati ya wafanyabiashara wa ndani na wageni.
“Kaangalie vyema suala ya wageni kufanya biashara inayofanywa na wenyeji… haiwezekani mgeni akawa machinga, sasa hawa vijana wetu watafanya nini? Kwa hiyo Waziri wa Biashara simamia hilo,” alisema Rais Samia.
Ameagiza wafanyabiashara wa Kariakoo watoe ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya kuchunguza majengo ya Kariakoo utakapoanza.
Rais Samia alisema soko lingine kubwa litajengwa katika eneo la Jangwani na wamachinga watapelekwa huko.
“Tumejipanga kujenga soko kubwa na zuri kama Kariakoo kwa hiyo ni maoni yetu baadhi ya wafanyabiashara, wanangu wamachinga tutawapeleka kule kufanya biashara kwa nafasi,” alisema.
Rais Samia ameiagiza Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) isipendelee wafanyabiashara, badala yake wote walipe kodi na kuwe na usawa katika soko.
Amewataka wafanyabiashara walipe kodi ili kupunguza kuomba misaada na kukopa fedha za kuendesha miradi ya maendeleo.
“Tushirikiane kwenye maeneo ya miundombinu, uendeshaji na ulipaji kodi… tusipolipa kodi na tukawaacha wachache walipe kodi na wabebe wengi wasiolipa hii ni hasara kubwa, lengo letu TRA itukusanyie trilioni (Shilingi)
nne kwa mwezi,” alisema Rais Samia.
Aliongeza, “mkifanya hivyo, tunailinda nchi yetu na kuwa ombaomba, tunailinda nchi yetu na mikopo, tunakopa kujenga… kuijenga nchi,mwingine anasimama anasema hii serikali kazi kukopa kwani tunakopa kununua sare za harusi? …mkitusaidia kila mfanyabiashara akilipa kodi mtatusaidia kupunguza kiasi cha kukopa.”