Samia ataja maeneo ushirikiano na Comoro

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na visiwa vya Comoro kukabili changamoto yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, afya na usafirishaji.

Pia, amesema kwa kuwa Tanzania na Comoro zina uhuru wa siasa, ni wakati sasa wa kupata uhuru wa kiuchumi.

Alisema hayo akiwa mgeni rasmi sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Comoro zilizofanyika katika uwanja wa Malouzini jijini Moroni kwa mwaliko wa Rais wa visiwa hivyo, Azali Assoumani jana. Comoro ilipata uhuru wake Julai 6, 1975.

Rais Samia alisema nyakati zinabadilika na zinakuja na changamoto na ni wazi kuwa Tanzania na Comoro zina changamoto zinazofanana.

“Comoro ni kisiwa ila Tanzania ni nchi yenye visiwa vidogo hivyo mabadiliko ya tabianchi yanatukabili wote, mabadiliko haya yamechangia kuongezeka kwa nyuzijoto, kuongezeka kwa maji ya chumvi ambayo yamekuwa yakila ardhi na kupoteza viumbe wa baharini, Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro ili kulinda ikolojia zetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.

Rais Samia alisema sekta nyingine ya kuiangalia na kuifanyia kazi zaidi kwa nchi hizo ni sekta ya afya ambayo ushirikiano wake umeimarika na mwaka huu kambi ya tiba inatarajiwa kufanyika Anjouan ikiwa ni kielelezo cha mshikamano wa kiutendaji.

“Mwaka jana Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilihudumia watu 2,700 kutoka visiwa vya Ngazija (Comoro)… inakisiwa kuwa Wacomoro wapatao 12,000 walipata huduma za afya Tanzania kwa mwaka 2024/2025, hii ni sekta ya kuiangalia na kuifanyia kazi kwa pamoja kwa karibu zaidi,” alisema.

Kuhusu sekta ya fedha, Rais Samia alisema imekuwa na mafanikio baada ya Benki ya Exim Tanzania kupeleka huduma hizo visiwani humo. Alisema benki nyingine ziko njiani kufungua matawi yao Comoro.

“Hii ni ishara ya kuaminiana baina ya sekta binafsi ya nchi ya Tanzania na Comoro,” alisema Rais Samia.

Alisema kukua kwa uhusiano hutegemea na mwingiliano wa watu na biashara baina yake na kwa kutambua hilo serikali ya Tanzania na Comoro zimechukua hatua za makusudi kuimarisha huduma ya usafiri na usafirishaji huku safari za boti zikiimarishwa

“Tuna mashirika mawili ya ndege, Air Tanzania na Precision yanayofanya safari kati ya Tanzania na Comoro na dhamira yetu ni kuongeza pia usafiri katika Bahari ya Hindi utakaotuunganisha, na nina furaha kuwajulisha kuwa Serikali ya Tanzania imedhamiria kufanya hivyo muda si mrefu,” alisema.

Rais Samia alitoa mwito kwa wana Comoro kujenga nchi yao kwa kudumisha umoja na kuendelea kuwa watulivu kwani nchi yao itajengwa na wao wenyewe na kwamba Tanzania ikiwa ndugu wa kweli itaendelea kuwaunga mkono katika nyakati zote nzuri na ngumu kwani udugu ni kufaana na si kufanana.

Alisema Tanzania na Comoro udugu wao si wa kuungaunga bali ni wa damu na kwamba ndiyo maana sasa si ajabu kuona Watanzania wakifanya tamaduni kama za ki Comoro mathalani, kufanya ada ya harusi siku saba.

“Tunayo jumuiya kubwa ya Comoro inayoratibu shughuli zao za kijamii Dar es Salaam, kuna msikiti wa Wangazija, makaburi ya Wangazija hii inaonesha kwamba watu wa Comoro wamejikita Tanzania kwa muda mrefu, inakadiriwa takribani ya Wacomoro 10,000 wako Tanzania na wengi wao wametangamana vema sana na Watanzania,” alisema.

Aliendelea, “… sasa hivi sio ajabu Tanzania na hasa Unguja kukuta tunafanya sherehe za ndoa za ada siku saba kama mnavyofanya upande huu, vilevile vyakula kama ladu, uji wa tapo na ndovi (ndizi) ni miongoni mwa vyakula vinavyopendwa pia kwa baadhi ya watu wetu bila kusahau kanga za shiromali na liwa au sandali inayopakwa usoni na ndugu zetu Wacomoro.”

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button